MFUMO MPYA WA KUPIMA UTENDAJI KAZI KUBAINI MIKOA NA HALMASHAURI ZINAZOONGOZA KUKWEPA KUTOA UFAFANUZI WA MASUALA YA KIUTUMISHI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema mfumo mpya wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma utatumika kubaini mikoa na halmashauri ambazo zinaongoza kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kuwasilisha barua kwa Katibu Mkuu UTUMISHI kuomba ufafanuzi wa masuala ambayo mikoa na halmashauri hizo zina uwezo wa kutoa ufafanuzi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na Wanasheria na Maafisa Utumishi kutoka katika Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, kabla ya kufungua kikao kazi cha maafisa hao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake. 

Mhe. Jenista amesema, mfumo huo utawaweka kwenye kundi la kutowajibika watumishi wote watakaosababisha mikoa na halmashauri zao kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kusingizia kuwa masuala hayo yanapaswa kutolewa ufanuzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. 

Mhe. Jenista amehoji kwanini mwajiri amuandikie barua Katibu Mkuu-UTUMISHI kuomba ufafanuzi wa jambo wakati mwajiri huyo anaye Afisa Utumishi ambaye akishirikiana vizuri na Mwanasheria, kwa kutumia nyaraka zilizopo wana uwezo mkubwa wa kulitolea uamuzi jambo ambalo linaombwa kutolewa ufafanuzi na Katibu Mkuu-UTUMISHI. 

“Maafisa Utumishi na Wanasheria mnapaswa kushirikiana katika kutoa ufafanuzi na kufanya maamuzi ya masuala ya kiutumishi kwa mujibu wa Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo ya kiutumishi iliyopo badala ya kukwepa jukumu hilo,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa amesema, kikao kazi hicho kimelenga kuibua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake hususani wakati wa kushughulikia masuala ya kinidhamu

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)