Idara ya Elimu Mkoa wa Dodoma imefikia maazimio yenye lengo la kuinua sekta ya Elimu kwenye Mkoa wakati wa kikao kazi kilichowashirikisha wadau mbalimbali wa Elimu chini ya Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule na Katibu Tawala wa Mkoa Bw. Ally Gugu kwenye ukumbi wa TAG - Mipango ulioko mkoani humo.
Miongoni mwa maazimio yaliyo fikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa Elimu kwenye kila Halmashauri ili kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu, utoaji wa chakula shuleni, kudhibiti utoro, ili kila shule kuhakikisha kila mwanafunzi anamudu mada inayofundishwa, kila mwanafunzi anayemaliza Elimu ya Msingi anaanza masomo ya kujiandaa na kidato cha kwanza wiki mbili baada ya kufanya Mitihani.
Mhe. Senyamule amesema matarajio ya Serikali ya awamu ya sita ni kuona maendeleo makubwa kwenye sekta ya Elimu kutokana na uwekezajj Mkubwa uliofanyika kipindi hiki hivyo ni wajibu wa wadau wote wa Elimu, ukiwa ni kukabiliana na changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo.
"Kikao hiki kimefuatia maagizo tuliyopeana ya kukaa vikao vya ngazi ya Vijiji, Kata, mpaka ngazi ya Wilaya ili kujadili namna ya kukabiliana na changamoto tunazoziona kwenye elimu. Serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye elimu hivyo inatarajia kuona maendeleo mazuri kwenye elimu. Nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na wadau, hakikisheni mnaongeza jitihada za kuthibiti utoro pia tuimarishe usimamizi katika ufundishaji kwa kutumia vitendea kazi ili kupandisha viwango vya ufaulu" Amesema Mhe. Senyamule.
Naye, Katibu Tawala Mkoa Bw Ally Gugu, ameongelea malengo ya Kitaifa ya kuinua ufaulu kwenye Mitihani ya Taifa ambapo kwa kidato cha nne ni kutoka ufaulu wa asilimia 32 hadi kufikia asilimia 50 na kwa kidato cha sita kutoka asilimia 99.6 hadi asilimia 100.
Pia amesisitiza juu ya wadau wa Elimu kuhakikisha wanakabiliana na changamoto zote zinazoikabili sekta ya Elimu ili lengo kuu la Serikali la kuinua sekta ya elimu liweze kufikiwa hasa kwa Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake mwenyekiti wa wakuu wa vyuo vya ufundi kanda ya ziwa Hezbon Mwera amesema kuwa taasisi yao inajishughulisha na mambo kadha wa kadha katika jamii kwa kibari walichopewa na OR- TAMISEMI katika mikoa Kumi ya Tanzania ikiwemo kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ndani ya vyuo vikuu.
“Sote tunatambua umuhimu wa vijana wetu kupata mafunzo ya elimu ya ufundi baada ya kuwa wamemaliza darasa la Saba, wakati wamemaliza wakiwa wanasubili matokeo ni vyema mkawapeleka huko”,amesema.