SERIKALI YASHAURIWA KUONGEZA WIGO WA BAJETI KWA WIZARA YA UWEKEZAJI VIWANDA NA BIASHARA.

MUUNGANO   MEDIA
0

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Biashara imeishauri Serikali kuongeza uwigo wa bajeti kwa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo hususani utafiti wa viwanda ambao ni nguzo ya maendeleo ya uchumi wa viwanda nchini. 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati hiyo cha Machi 21, 2023 Mhe. Mhandisi Ezra Chiwelesa (Mb.) wakati Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ikiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa Kamati hiyo Bungeni Dodoma.

Nao Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni mbalimbali yaliyolenga kuwezesha utekelezaji wa miradi hususani miradi ya utafiti wa viwanda ili viendane na wakati, teknolojia ya kisasa na mahitaji ya sekta zote za uzalishaji ikiwemo kilimo na mifugo, uwezeshaji wa wajasiriamali na utafutaji wa masoko ya nje ya bidhaa za Tanzania.

Akijumuisha,maoni na mapendekezo ya Kamati hiyo, Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Wizara itaendelea kutekeleza kikamilifu ushauri na maelekezo ya Kamati hiyo ili kuendeleza sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akiwasilisha Taarifa hiyo amesema kuanzia Julai 2022 hadi Febuari 2023, Wizara imefanikiwa kusajili jumla ya miradi mipya 204 yenye jumla ya dola za Marekani milioni 3,591 na kutoa ajira 31,531. 

Aidha, amesema Wizara imehamasisha ujenzi na upanuzi wa viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo ikiwemo Viwanda vya Sukari (Bagamoyo; Mkulazi, Kilombero na Kagera), Serengeti Breweries – Moshi pamoja na Kiwanda cha mbolea cha Intracom Dodoma na Minjingu Arusha ili kuleta tija katika kilimo.

Aidha, amesema Wizara imeendelea kutekeleza Miradi ya Kimkakati na ya Kielelezo kwa manufaa ya Taifa ikiwemo Mradi wa Magadi Soda - Engaruka, Makaa ya Mawe - Mchuchuma, Chuma - Liganga, Chuma ghafi (iron ore) Maganga Matitu na Makaa ya Mawe - Katewaka, pamoja na ujenzi wa kongani za viwanda na maeneo maalumu ya uchumi ikiwemo Kongani ya viwanda ya Kwala -Pwani, Mkulazi – Morogoro, Nala – Dodoma na Bagamoyo.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)