Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mpimbwe Catherine Mashalla ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuweka nguvu katika suala la elimu na uhamasishaji wa chanjo ya Surua kwani hatua hiyo imesaidia kuvuka lengo la Halmashauri ambapo walikuwa na lengo la kuchanja watoto 29, 000 lakini kutokana na hamasa hiyo wamechanja watoto 43,384.
Amebainisha hayo Wilayani Mlele Mkoani Katavi wakati wa kuhitimisha kampeni ya siku 14 ya Elimu na Uhamasishaji wa chanjo ya Surua iliyoendeshwa kwa njia ya magari na njia ya simena iliyoanza Febururi 24.2023 hadi Machi 9 2023 ikiwa ni utekelezaji wa kampeni hiyo.
“Nina shukuru sana kama Halmashauri tumepata Support ya kutosha kabisa kutoka Wizara ya Afya na kwa maana hiyo sasa tumeweza kufikia mafanikio haya hata ile trend ya kesi mpya nayo imeshuka leo tunazungumzia 56 kutoka mia na zaidi kuna maendeleo makubwa, wale wanaokwenda kulazwa sasa hivi tuna namba tu ya watu wawili, hata wale tuliowalenga halmashauri kuwachanja walikuwa ni 29,000 leo hii tunazungumzia zaidi ya elfu arobaini na tatu ni mafanikio makubwa”amesema Mashalla.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Halmashauri ameomba nguvu kubwa iliyotumika katika elimu na hamasa ya chanjo ya Surua itumike pia katika uhamasishaji kwa jamii kuhusu masuala ya lishe ili kupunguza tatizo la udumavu na utapiamlo katika eneo halmashauri ya Mpimbwe na Katavi kwa Ujumla.
Mganga Mkuu Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi Martin Lohay amesema watu waliogundulika na maambukizi ya Surua katika halmashauri hiyo ni 1967 huku akiipongeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkoa pamoja na Wizara ya Afya kwa kusaidia katika utoaji wa elimu na hamasa ya chanjo ya Surua.
Ikumbukwe kuwa katika kampeni ya siku 14 ya Hamasa ya chanjo na Elimu ya Surua Halmashauri ya Mpimbwe, jumla ya kaya 15,750 zilitembelewa, na magari ya matangazo na sinema kufika katika maeneo ya Majimoto, Kibaoni, Chamalendi, Mbende,Mwamapuli, Kasansa, Usevya, Ikuba, na Mamba huku watoto waliopona Surua ni 1749 kati ya wagonjwa 1967 na waliofariki hadi sasa ni watoto 16.

