AINA 11 YA WADUDU RAFIKI YASAJILIWA ILI KUPUNGUZA MATUMIZI YA VIUATILIFU VYA VIWANDANI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, amesema kuwa mamlaka hiyo imefanikiwa kusajili jumla ya aina 11 ya wadudu rafiki ili kupunguza matumizi ya viuatilifu vya viwandani.

Prof. Ndunguru amebainisha hayo leo Machi 1,2023 Jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Sambamba na hayo emeongeza kuwa TPHPA imedhibiti milipuko ya panya katika mikoa ya mbalimbali ambapo jumla ya eneo la ekari 122,190 liliokolewa na uvamizi wa panya hao huku mafunzo ya namna ya kuwatambua aina ya panya na mbinu za kudhibiti yakitolewa kwa wakulima.

Aidha Prof. Ndunguru hakusita kuzungumzia mafanikio waliyo yapata kuanzia mwezi Julai 2022 hadi Februari 2023 ambapo amesema kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo imefanya uchambuzi wa sampuli za udongo takribani 1300 kutoka kwenye mashamba ya “Block farming” na matokeo ya uchambuzi huo yatawezesha kutoa ushauri.

“Ili kuwezesha biashara ya mazao, sampuli 40 zilifanyiwa uchambuzi kwenye mazao mbali mbali, sampuli zote zilikidhi viwango na biashara ya mazao ilifanyika,”amesema.

Amesema mamlaka hiyo imeendelea kuwajengea uwezo wakaguzi wa Mimea na mazao waliopo katika mipaka ya nchi jumuia ya Afrika mashariki kwa njia ya mafunzo.

“Jumla ya wakaguzi 72 wa Afya ya Mimea kutoka vituo vya Rusumo, Kabanga, Mutukula, Mrusagamba, Kibirizi, Mabamba, Manyovu, Bukoba port, Mwanza Port, Sirari, Holili, Tarakea na Namanga, Tanga port, Horohoro, Dares Salaam port, Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere, Mtwara port, Uwanja wa ndege wa Songwe, Tunduma, Kasumulo na Mtambaswala,”amesema.

Pia ametaja malengo yao kuwa ni kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara viuatilifu kwa watengenezaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji ili kupunguza athari ya kuwepo kwa viuatilifu bandia. 

“Katika kipindi hiki, mamlaka inafanya ukaguzi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mbeya, Njombe, Iringa, Songwe, na Morogoro,”ameesema.

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imeundwa na sheria namba 4 ya 2020 (Plant Health Act. No. 4) ikiwa ni muungano kati ya TPRI (Sheria Na. 18 ya 1979) na PHS (Sheria Na. 13 ya 1997) huku ikianza rasmi Julai 2022.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)