KATIBU MKUU SANGA AJA NA MWAROBAINI CHANGAMOTO YA UKUSANYAJI KODI YA PANGO LA ARDHI

MUUNGANO   MEDIA
0


Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amehaidi kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa ukusanyaji mapato yatokanayo na pango la ardhi kama ilivyo mifumo ya kisasa inayotumiwa na mamlaka za maji safi na mazingira hapa Nchini.

''Ili kuwa na mafanikio makubwa ni lazima tujue idadi ya wamiliki wa ardhi nchini kwa kuwaingiza kwenye mifumo ili tuweze kujua kiwango cha mapato yatokanayo na kodi ya ardhi hapa Nchini''Alisisitiza Katibu Mkuu mteule Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga.

Mhandisi Sanga amesema hayo leo tarehe 28 Februari wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kati yake na Katibu Mkuu anayemaliza muda wake Dkt. Alla Kijazi kufuatia kuteuliwa kwake kuongoza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi uteuzi uliofanywa hivyi karibuni na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akitoa uzoefu wake katika mifumo ya ukusanyaji mapato kupitia Wizara ya maji na mamlaka zake Mhandisi Sanga amesema walifanikiwa kuwa na mifumo imara baada ya kuachana na mifumo kutoka nje ya nchi na kuwaamini wataalam wa ndani ambao wamefanikiwa kutengeneza mifumo imara ya ukusanyaji miamala ya maji.

Ni kwa muktadha huo Katibu Mkuu Sanga akaimiza kutumia wataalam wa mifumo wandani na kuamini watendaji wengine wa sekta ya ardhi kwa kuwapa nafasi ili waweze kuonesha uwezo wao akichagiza kuwa yeye anatabia ya kuamini watu anaofanya nao kazi.

Naye Katibu Mkuu anayemaliza muda wake Dkt. Allan Kijazi amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na kiongozi huyo mpya ili kuendeleza kazi kubwa ambayo yeye na wenzake wamekuwa wakiendelea nayo hadi sasa wakati anamaliza muda wake.
Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)