WEO's ARUSHA DC WAPATA MGAO WA PIKIPIKI ZA SERIKALI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Maafisa watendaji wa kata 8 halmashauri ya Arusha wamekabidhiwa pikipiki zilizotolewa na serikali kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi nchini.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pikipiki hizo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amesema kuwa pikipiki hizo ni vifaa muhimu kwa Maafisa hao zinazokwenda kumaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu kuwafikia wanachi ili kutoa huduma. 

Ameweka wazi kuwa, kata hizo 8 ziko maeneo ya pembezoni zikiwa na maeneo makubwa ya kiutendaji hivyo Maafisa hulazimika kutembea muda mrefu kuwafikia wananchi kutoa huduma jambo ambalo linakwenda kumalizika sasa.

Aidha amewataka Maafisa hao kutumia pikipiki hizo kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa na serikali ya kuwahudumia wananchi na si vinginevyo huku akiwasisitiza kuzitunza na kuzithamini kwa kutambua kuwa ni mali ya Umma.

"Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuwatahamini Maafisa Watendaji wa kata, kwa kuwa wao ndio wanawahudumia wananchi moja kwa moja, Watendaji mnalo deni sasa, mkatumie vifaa hivi kulingana na malengo yaliyokusudiwa na si kwa matumizi binafsi". Amesisitiza Mkurugenzi Msumi.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya kichama Arumeru, Komredi Noel Severe, ameipongeza serikali kwa kuteketeleza Ilani ya Chama hicho kwa vitendo, kwa kuhakikisha watumishi wanapata vitendea kazi vitakavyorahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.

"Serikali inawategemea, mmepata usafiri, tumieni muda mwingi kutatua kero na changamoto za wananchi kwenye maeneo ya vijiji na vitongoji vyenu kwa wakati, kwa kufanya hivyo, tutafikia malengo ya serikali ambayo ndio maagizo ya Ilani". Amesisitiza Mwenyekiti huyo wa CCM.

Hata hivyo Maafisa Watendaji hao, wameipongeza serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwapatia usafiri, jambo ambalo wamekiri lilikiwa ni changamoto kubwa iliyokwamisha utendaji kazi katika maeneo yao.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)