Na WyEST,Butiama
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda leo Jumamosi Februari 18, 2023 ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo Cha VETA cha Wilaya ya Butiama.
Katika ziara hiyo Mkenda ameelekeza uongozi wa VETA Mara ambao ni wasimamizi wa ujenzi huo kuhakikisha wanashirikiana na Taasisi za Serikali zilizo jirani na Chuo hicho katika kazi mbalimbali za kukamilisha Ujenzi hususan kazi za nje.
"Hapa ujenzi karibu umekamilika lakini kazi za nje bado, tafuteni taasisi za kushirikiana nazo kama JKT wako hapo jirani kuandaa njia na mazingira kwa ujumla," amesema Prof. Mkenda.
Mkenda amemtaka Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi huo kuhakikisha ubora wa majengo mbalimbali ikiwemo karakana unasimamiwa na kuondoa upungufu unaoonekana.
Katika hatua nyingine Mkenda ameelekeza Chuo hicho kitakapoanza kuhakikisha kinatoa mafunzo yanayoendana na mazingira na uhitaji wa jamii.
"Hapa jirani kuna chuo cha mafunzo ya ufundi miundo mbinu yake imechakaa hivyo oneni pia njia ya kushirikiana nao kuendeleza utoaji mafunzo kutumia maabara za hapa, huko tunakoenda elimu yetu itajikita katika ujuzi hivyo vyuo hivi na shule za ufundi zitahitajika sana, shirikianeni," ameongeza Profesa Mkenda.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Moses Kaegele ameongeza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu na Wilaya wamekuwa karibu sana katika kufuatilia ujenzi huo na kwamba wataendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kazi inakamilika hasa kwa kuwa fedha za kukamilisha tayari zimetolewa na Wizara.
Naye Mbunge wa Butiama Mhe. Jumanne Sagini ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Chuo hicho na kuomba kuongezwa nguvu katika usimamizi ili ujenzi ukamilike na mafunzo kuanza kutolewa huku akimshukuru Waziri wa Elimu Profesa Mkenda kwa kutekeleza ahadi ya kutembelea na kukagua ujenzi wa VETA Butiama.


