Na.Elimu ya Afya kwa Umma,Katavi
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu ameagiza wakuu wilaya na mikoa kote nchini kuhakikisha wanawachukulia hatua wazazi na walezi wote ambao watashindwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya Surua.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya na kuzindua kampeni ya kuongeza kasi na hamasa ya chanjo ya Surua kwa Halmashauri ya Mpimbwe Wilayani Mlele mkoa wa Katavi.
“Kwa mamlaka niliyopewa nataka wakuu wa mikoa kuwatafuta watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano ambao hawajapa chanjo ya Surua na kuhakikisha wanapatiwa chanjo hiyo na kukamilisha ratiba ya chanjo hiyo ni kwa mujibu wa sheria”amefafanua Mhe.Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameuagiza Mkoa wa Katavi kuhakikisha unachanja watoto wote ambao hawajapata chanjo ambapo ameongeza kuwa serikali itaendelea kuongeza fedha kwa ajili ya utoaji wa elimu umuhimu wa chanjo ambapo pia kampeni ya chanjo nyumba kwa nyumba itaanza ili kuongeza kasi ya kuchanja na kuweza kupunguza vifo.
Ikumbubukwe kuwa kuna watoto zaidi ya 400,000 nchini ambao hawajapata chanjo ya ugonjwa wa Surua na vifo vilivyoripotiwa hadi sasa ni vifo 13 kati ya hivyo vifo 11 vimetokea kwenye jamii, vifo 2 hospitalini na hivyo ni kutokana na wagonjwa kuchelewa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya