WAZIRI KAIRUKI ATOA MAAGIZO YANAYOGUSA VIONGOZI NA WATUMISHI

MUUNGANO   MEDIA
0

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki ametaka viongozi kuongeza kasi katika uchukuaji wa hatua dhidi ya wale wote wanaokwenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo Februari 28,2023 wizarani jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kikao cha Menejiment cha mapokezi ya viongozi wapya wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Amesema,katika kusimamia mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa kuna changamoto za kiutumishi ambazo zinatokea, lakini viongozi wamekuwa wagumu kuchukua hatua stahiki kwa watumishi hao, hivyo kuanzia sasa kiongozi ahakikishe anachukua hatua stahiki za kinidhamu katika maeneo ambayo yanaweza kuleta taswira hasi kwa Serikali.

Aidha, amewataka viongozo wote kuacha kufanya kazi kwa mazoea,kwani kunazorotesha jitihada za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia amesisitiza kufuatilia na kufanya tathmini (Performance Tracking) ya utendaji kazi wa watumishi na kuona matokeo ya wale ambao wanawasimamia ili kama sehemu kunalega au kuna mabadiliko hatua zichukuliwe.

"Mtumishi anaweza kuwa vizuri na mchapa kazi kwa wakati fulani,lakini baada ya muda unakuta amebadilika utendaji kazi wake unazorota, sasa hapo ndipo mnapotakiwa kufuatilia na kufahamu mabadiliko hayo yametokana na nini na kumuwezesha kuendelea na majukumu kikamilifu,"amesisitiza Waziri Kairuki.

Pia amewataka viongozi hao kushauriana na kushirikishana katika utendaji kazi wao ili kuleta uelewa wa pamoja katika kuwahudumia wananchi jukumu ambalo limenabeba taswira nzima ya Wizara ya OR-TAMISEMI.

Mhe. Kairuki amewataka viongozi hao kusimamia ujibuji wa hoja za Ukaguzi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kuwa zinapungua au kufungwa kabisa na sio kuziacha hoja hizo ziendee na kusababisha dosari kwa Serikali kila wakati.

Wakati huo huo Mhe. Kairuki amesisitiza usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili thamani ya fedha ionekane na iweze kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)