MHE. MHAGAMA AWATAKA WATUMISHI WA OFISI YAKE KUTOA USHIRIKIANO WA KIUTENDAJI KWA VIONGOZI WAPYA ILI KUENDELEA KUUBORESHA UTUMISHI WA UMMA

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa watumishi wa ofisi yake kuendelea kutoa ushirikiano wa kiutendaji kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi walioteuliwa na kuapishwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutumikia ofisi hiyo.

Mhe. Jenista ametoa wito huo leo jijini Dodoma, wakati wa hafla fupi ya kuwapokea viongozi hao walipowasili ofisini kwa ajili ya kuanza kazi rasmi mara baada ya kuapishwa jana na Rais wa Jamhuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema ushirikiano kwa viongozi hao kutoka kwa watumishi utawawezesha kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutoa mchango katika Utumishi wa Umma kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imepata viongozi wenye sifa stahiki kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kiutendaji, hivyo hatuna budi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika kufikia maono ya Rais wa Awamu ya Sita ya kuuboresha Utumishi wa Umma nchini.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, viongozi hao wateule wataendeleza pale walipoishia watangulizi wao katika kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi katika kutoa huduma bora.

Kwa upande wake, Naibu Waziri mteule, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wote na kuongeza kuwa, atahakikisha anasimamia haki katika kufanya kazi.

Mhe. Ridhiwani amesema, moja ya jukumu lake ni kumsaidia Waziri wake Mhe. Jenista Mhagama kutekeleza jukumu la kusimamia utumishi wa umma na utawala bora kwani kwa kufanya hivyo atakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)