Na Gideon Gregory, Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Benny Ndomba ametoa rai na kuwakumbusha wadau wote wa TEHAMA nchini kushiriki kikamilifu katika kikao kazi cha tatu cha serikali Mtandao kwa kufanya usajili kupitia mfumo wa TSMS (https://tsms.ega.go.tz).
Mhandisi Ndomba ametoa rai hiyo Jijini Dodoma katika kikao na waandishi wa habari leo Februari 6,2023 kitakacho fanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 8-10 katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama.
Amesema lengo la kikao hicho ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa serikali Mtandao ili kujadili juu ya mafanikio, changamoto pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza serikali Mtandao nchini pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA katika taasisi za umma sambamba na kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Takribani wadau 1000 wa serikali mtandao kutoka mashirika na taasisi za umma wakiwemo maafisa mashuuri, wajumbe wa bodi, wakuu wa vitengo vya TEHAMA, maafisa TEHAMA, maafisa Rasilimali watu, maafisa mipango, maafisa mawasiliano, wahasibu pamoja na watimiaji wote wa mifumo ya TEHAMA seeikalini wanatarajia kushiriki,”amesema Ndomba.
Aidha ameongeza kuwa kikao hicho kitaongozwa na kauli mbiu isemayo “Mifumo Jumuishi ya TEHAMA kwa utoaji huduma bora kwa Umma ” ikiwa ni kuhamasisha taasisi za umma kutumia mifumo jumuishi inayowasiliana katika utendaji kazi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Mamlaka ya serikali Mtandao (eGA) ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza juhudi za serikali Mtandao pamoja na kuhimiza uzingatiwaji wa sera, Sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali Mtandao katika taasisi za umma ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA yanazingatiwa katika taasisi hizo,”amesema.
