WADAU WA MADINI WAIPONGEZA SERIKALI USIMAMIZI WA UKUTA WA MIRERANI

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Wadau wa madini wakiwa ni pamoja na wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ya tanzanite wanaoendesha shughuli zao ndani ya ukuta wa Mirerani, Wilayani Simanjiro mkoani Manyara wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini, Tume ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na usimamizi mzuri wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ndani ya ukuta huo hali iliyopelekea kuimarika kwa usalama na kupungua kwa vitendo utoroshaji wa madini.

Wadau wamezungumza hayo leo Februari 13, 2023 kwenye mahojiano maalum ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia namna shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ya vito zinavyochangia kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.

Akizungumza  kwa niaba ya wadau hao, Mkurugenzi wa Kampuni inayojihusisha na  uchimbaji wa madini ya tanzanite ya Franone, Mjiolojia Vitus Ndakize amesema kuwa tangu kujengwa kwa ukuta wa Mirerani kumekuwepo na mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama kwenye shughuli za uchimbaji, biashara na usafirishaji wa madini  sambamba na kupungua kwa vitendo vya wizi kwenye migodi ya madini.

Ameongeza kuwa mabadiliko mengine ni pamoja na kupungua kwa gharama za uendeshaji kwa kuwa huduma zote za uthaminishaji na masoko ya madini zinapatikana ndani ya eneo la Mirerani.

“Kabla ya ujenzi wa ukuta huu, wachimbaji wa madini walikuwa wanahangaika na kutafuta masoko ya kuuzia madini yao, hali ambayo ilikuwa ni hatari, wakati mwingine walikuwa wakiuza kwa bei ndogo kutokana na kutokujua thamani halisi ya madini lakini mara baada ya kujengwa kwa ukuta madini yanathaminishwa na wataalam wa Tume ya Madini, kuuzwa kwa bei halisi huku Serikali ikipata kodi na tozo mbalimbali,”amesema Ndakize.

Naye Meneja wa Mgodi wa Gem & Rock Venture,  Mhandisi Enock Nanyaro ameongeza kuwa uwepo wa ukuta wa Mirerani umechangia kwa kiwango kikubwa cha uzalishaji wa madini ya tanzanite katika mgodi huo na kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo la Mirerani.

Wakati huo huo akizungumza kwa niaba ya wanawake wanaojihusisha na biashara ya madini ya tanzanite katika ukuta huo, Mwenyekiti wa  Wanawake wa Mirerani Tanzanite (MIWOTAMA),  Joyce Mkilanya ameongeza kuwa kumekuwepo na maboresho kwenye eneo la ukaguzi ambapo watu wamekuwa wakikaguliwa kwa kuzingatia utu na heshima.

Awali akielezea namna usimamizi wa shughuli za uchimbaji na uthaminishaji wa madini ndani ya ukuta wa Mirerani, Afisa Madini Mkazi wa Mirerani, Mhandisi Menard Msengi amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imekuwa ikisimamia suala la usalama kuanzia kwenye lango la kuingia, uchimbaji na uthaminishaji wa madini na lango la kutokea lengo likiwa ni kuzuia mianya ya utoroshaji wa madini huku Serikali ikipata mapato yake.

Ameongeza kuwa ofisi yake hutoa vibali vya usafirishaji wa madini nje ya nchi kwa wafanyabiashara wa madini ambao hupeleka madini yao kuuza nje ya nchi ambapo wengi wao hupeleka madini katika nchi za Marekani na India.

Ameendelea kusema kuwa kutokana na usimamizi mzuri wa madini ya tanzanite katika eneo la Mirerani katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu ofisi yake imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.7.

Aidha, amesema kuwa sambamba na makusanyo ya maduhuli migodi ya madini katika eneo la Mirerani imeendelea kuboresha huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule na vituo vya afya.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Msengi amewataka wawekezaji zaidi kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ya tanzanite.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)