Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka Watendaji wa Kata na Viongozi wa Mikoa wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kutumia vitendea kazi wanavyokabidhiwa na serikali katika kuwafikia wananchi kwa urahisi, kuwasikiliza, kuwahudumia,kufuatilia miradi ya maendeleo na siyo kutumia kwa manufaa binafsi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi magari 54 kwa kwa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Pikipiki 916 kwa Watendaji Kata zilizotolewa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Hafla iliofanyika katika ukumbi wa Halmshauri ya Jiji la Dodoma – Mtumba leo tarehe 14 Februari 2023. Amewaagiza maafisa watendaji kutambua na kushughulikia changamoto za wananchi kwa kuhakikisha vikao na wananchi katika ngazi ya Vijiji na Mitaa vinafanyika kama inavyopaswa.
Makamu wa Rais amewaasa Maafisa Watendaji kata kuacha uzembe katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli nyingine za kijamii. Amesema utoaji wa vitendea kazi hivyo pamoja na mambo mengine unalenga kuongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo wanayosimamia. Pia amesema ni muhimu kuzingatia uhifadhi wa mazingira kwa kutoa hamasa kwa wananchi ili wawe mstari wa mbele katika shughuli za uhifadhi ikiwemo kupanda miti na usafi wa mazingira ili kuwepo na maendeleo endelevu.
Pia Makamu wa Rais amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha fedha kiasi cha Shilingi laki moja inayopaswa kutolewa kwa Maafisa Watendaji wa Kata kama posho ya madaraka inatolewa kwa wakati na kupewa kipaumbele kabla hazijalipwa posho za vikao vingine vya Halmashauri.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha mfumo na utendaji wa Serikali za Mitaa, kwa kuzingatia misingi ya Kikatiba na Kisheria iliyopo kwa kutambua kwamba, mfumo wa Serikali za Mitaa, ndio njia pekee ya kusogeza huduma karibu na wananchi lakini pia kuwashirikisha wananchi katika kuamua, kupanga na kuchagua vipaumbele vya maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.