VIFO VYA WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA MITANO VIMEPUNGUA NCHINI

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Gideon Gregory, Dodoma.

Tafiti zinaonesha kuwa kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa Mwaka 2022 kimefika vifo 43 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai ukilinganisha na vifo 67 kwa kila Watoto 1,000 waliozaliwa hai ilivyokuwa kwenye Utafiti uliofanyika mwaka 2015/2016.

Hayo yamesema leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa matokea muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa Mwaka 2022 uliofanyika katika ofisi za Taifa ya Takwimu Jijini Dodoma.

"Kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwezi mmoja vimepungua kutoka vifo 37 mwaka 1990 hadi vifo 18 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 ambapo vimepungua kwa asilimia 51." Amesema Ummy Mwalimu 

Pia, Waziri Ummy amesema Vifo vya Watoto chini ya mwaka mmoja navyo vimepungua kutoka vifo 65 mwaka 1990 hadi vifo 28 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 ambapo kwa jumla ni punguzo la asilimia 56.

"Haya ni matokeo makubwa ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea katika mpango wa Tatu wa maendeleo ya Taifa ambao unalenga kupunguza vifo vya Watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi vifo 40 katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai ifikapo mwaka 2025/26." Amesema Waziri Ummy .

Katika kuonesha umuhimu wa Tafiti Waziri Ummy amesema matokeo haya muhimu ya Utafiti yataiwezesha Serikali ya awamu ya Sita inayoogozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika mipango ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa hasa katika eneo la Afya ya Uzazi na Mtoto.

"Utafiti huu ni moja kati ya tafiti muhimu katika sekta ya afya kwani hutoa tathmini ya ubora wa huduma zinazotolewa nchini, changamoto zilizopo katika sekta ya afya na kushauri namna ya kukabiliana nazo." Amesema Waziri Ummy


"Kwa mwaka 2022 matokeo yanaonesha 3.3% ya watoto chini ya umri wa miaka mitano (5) wana ukondefu (wembamba kwa kulinganisha na kigezo cha urefu wao) ikilinganishwa na 4.5% kwa Utafiti wa mwaka 2015/16." Amesema Waziri Ummy 


Mwisho

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)