SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA MAZINGIRA SALAMA YA BIASHARA

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Serikali imewahakikishia wafanyabiashara kutoka Nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama, bora na rafiki.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi alipofunga Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya lililofanyika jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 23 – 24 Februari 2023. 

Dkt. Mwinyi alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.

“EU imekuwa mwekezaji mkubwa nchini Tanzania na imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ufanyaji biashara kati yake na Tanzania, lengo la serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ni kukuza na kuendeleza sekta binafsi yenye nguvu, hivyo natoa rai kwenu kuwekeza kwa wingi kwani mazingira ni bora na salama,” alisisitiza Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi aliongeza kuwa Serikali imejikita katika kukuza uwekezaji kupitia sekta za kilimo, uchumi wa buluu, madini, usafirishaji, miundombinu, utalii na nyingine nyingi na kuwasihi wafanyabiashara wapatao 400 kutoka EU kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)