NAIBU WAZIRI KIKWETE AELEKEZA EKARI 2,390 ZILIZOTOLEWA NA RAIS SAMIA KUPANGWA NA KUMILIKISHWA

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara kuweka mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kuwapatia hati wakazi wa eneo la ekari 2,390 zilizotolewa na Mhe. Rais katika Bonde la Kiru Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kikwete ametoa maelekezo hayo kwa Kamishna huyo Bw. Joseph Batinamani wakati alipofanya ziara leo tarehe 12 Februari 2023 katika kijiji cha Kiru Dick halmashauri ya wilaya ya Babati mkoa wa Manyara.

Kikwete ametoa maelekezo hayo kutokana na mgogoro uliopo kati ya wakazi wa Kijiji cha Kiru Dick Valley wilayani Babati Mkoa wa Manyara na muwekezaji wa kampuni ya Hamir Estate Ltd inayojishughulisha na kilimo cha miwa ambaye ni wamiliki wa awali wa Mashamba hilo.

Aidha, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kumega ekari 2,390 ambazo zilikuwa zikimilikiwa kihalali na Kampuni ya Hamir Estate Ltd kwenye mwaka 1999 na kuwapa wananchi ili kumaliza mgogoro huo.

“Natoa maelekezo kwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara kulitambua eneo hili na kuliwekea mpango wa matumizi ya ardhi. Tambueni maeneo ambayo yanafaa kwa shughuli za kilimo na shughuli za wananchi natambueni maeneo ambayo tutawapanga wananchi ambao ambao hawana kabisa mashamba” Amesema Kikwete.

Pamoja na maamuzi hayo Kikwete amewaonya wakazi wa eneo hilo kujiepusha na uvunjifu wa amani kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu ambavyo vimekuwa vikiendelea katika eneo hilo na badala yake amewataka kuonesha ushirikiano kwa muwekezaji kwa kuwa tayari ameishatoa ekari 2,390.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere amewataka wakazi wa eneo hilo kuwa nasubira wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais ili wananchi hao waweze kupangwa na kumilikishwa maeneo hayo na kupatiwa hati za umiliki wa ardhi.

“Ni kweli Mhe. Rais tayari ameishatoa eneo la ekari 2,390 lakini bado inabidi taratibu zifanyike kama ambavyo umeelekeza waweze kupangwa, kupimiwa na kupatiwa hati ili kila mmoja amiliki sasa eneo lake” Alisema Makongoro.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)