DC NACHINGWEA AZINDUA ZOEZI LA UFUNGAJI VISUKUMA MAWIMBI KWA TEMBO

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohamed H. Moyo amezindua zoezi la ufungaji visukuma mawimbi "GPS Satellite Collars" kwa makundi ya Tembo wanaosumbua wananchi katika Vijiji vya Wilaya za Nachingwea, Liwale na Tunduru.

Zoezi hilo linaloendeshwa na TAWIRI na TAWA kwa kushirikiana na viongozi wa Wilaya na vijiji limeanza kutekelezwa Februari 10, 2023 na linalenga kusaidia kupata taarifa za wakati kuhusu mienendo na mahali yalipo makundi ya tembo na hivyo kurahisisha ufuatiliaji na kuzuia wanyamapori hao wasilete madhara kwa watu, makazi na mashamba yao.

Katika zoezi hilo jumla ya visukuma mawimbi vitano (05) vinatarajiwa kufungwa kwenye makundi ya Tembo, ambapo hadi kufikia Februari 12, 2023 jumla ya visukuma mawimbi "GPS Satellite Collars" vitatu (03) vilifungwa kwenye makundi matatu ya tembo katika maeneo ya Milola/Mitamba (Wilaya ya Lindi vijijini), Mkutano (Liwale) na Ngolanga ambayo ni shoroba ya Selous - Niassa (Tunduru).

Aidha, visukuma mawimbi viwili (02) vilivyobaki vinatarajiwa kufungwa katika maeneo ya Wilaya hiyo yenye changamoto kubwa zaidi. Vilevile, TAWIRI na TAWA zitaendelea kufunga visukuma mawimbi (GPS Satellite Collars) kwenye makundi mengine ya tembo ili kuwezesha vikosi vya askari wanaofanya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kufika kwa haraka katika maeneo ya karibu na vijiji tembo hao watakapoonekana. 

Akihitimisha uzinduzi wa zoezi hilo la ufungaji wa visukuma mawimbi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea ameipongeza Serikali kupitia taasisi zake za TAWIRI na TAWA kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Vilevile, alibainisha kuwa uongozi wa Wilaya uko tayari kuendelea kushirikiana na wataalamu wa uhifadhi katika kutatua changamoto hii.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)