NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA Chama Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kitaendelea kuenzi na kuthamini juhudi za waasisi katika kuimarisha Chama.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed 'Dimwa',katika ziara yake ya kuwatembelea waasisi wa Chama katika Mkoa wa Kusini Unguja Kichama.
Alisema historia halisi ya Ukombozi wa waafrika wa Zanzibar inatokana na juhudi za wazee hao walioshiriki katika harakati za Mapinduzi ya mwaka 1964 na wazaa fikra za Muungano wa nchi mbili na mwaka 1977 wakaviungamisha Vyama vya ASP na TANU ikazaliwa CCM.
Dkt.Dimwa,alieleza kuwa mafanikio ya kisiasa,kiuchumi na kimaendeleo yaliyofikiwa hivi sasa nchini yametokana na misingi imara iliyowekwa na wasisi hao.
Alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kukutana na wazee walifanya kazi za kuimarisha Chama bila kujali maslahi binafsi.
Alisema wazee hao wana utajiri wa maarifa ya kufundisha historia ,itikadi na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi.
"Kupitia ziara hii tumejifunza na kusikia mengi mazuri kutoka Kwa Wazee wetu ambao ndio chimbuko la uhuru,maendeleo,amani na mshikamano wetu kwa Sasa".alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Alieleza kuwa maana ya chama kurudi kwa Wanachama wenyewe ni pamoja na kuwatembelea waasisi hao ili makundi ya Wanachama wote wapate nafasi sawa ya kunufaika na fursa za Chama.
Akitoa wito Kwa Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali kuendeleza utamaduni wa kufanya ziara za kuwatembelea Wananchi katika maeneo yao ili kuratibu changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.
Naye Hassan Ussi Hassan ambae ni muasisi wa chama cha mapinduzi kutoka katika kijiji cha Makunduchi amesema anamshukuru Naibu Katibu Mkuu kuja kumuona na kumjulia hali kwani kitendo hicho kinajenga umoja na mshikamano kama ulivyojengwa katika kipindi cha chama cha ASP.
Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa wilaya ya Kusini Unguja Haji Abdalla Mzee ameshauri kuwa ipo haja ya kufanya utafiti ili kuweza kutekeleza mambo mengi ambayo CCM imeahidi kwa wananchi.
Waasisi waliotembelewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mzee Khatibu Ramadhan Iddi ambae alikuwa Mwenyekiti wa CCM jimbo la Tunguu,Mzee Haji Abdalla Haji alikuwa mwenyekiti wa wilaya ya kusini,pamoja na Hassan Ussi Hassan ambae ni muasisi wa chama cha mapinduzi.
MWISHO