
Na Anitha Jonas – COSOTA, Dar es Salaam,
Taasisi ya Hakimiliki Tanzania
(COSOTA) ya jibu hoja zilizotolewa na taasisi ya Creative Industry Network
Tanzania (CNIT) kwa kushirikiana na Twaweza na kusisitiza suala la ukusanyaji
na ugawaji wa mirabaha siyo la uanaharakati ni suala la kisheria.
Kauli hiyo imetolewa leo
Februari 22, 2022 na Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki
Tanzania Doreen Anthony Sinare katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Akiendelea kuzungumza Afisa
Mtendaji Mkuu huyo alieleza kuwa Kanuni ya usajili wa wanachama na kazi zao
inataka wabunifu wa Hakimiliki, Asasi na Makundi yanayojihusisha Hakimiliki
kujisajili COSOTA ili waweze kutambuliwa , hivyo taasisi ya CNIT wala Mkurugenzi
Mtendaji wake Robert Mwampembwa pamoja na Twaweza hazitambuliki na COSOTA.
"Kwa mdau yoyote
aliyekuwa na maswali, hoja au maoni kuhusu mgao wa mirabaha uliyofanyika hivi
karibuni anakaribishwa ofisini kuuliza na siyo kuanza kufanya upotoshaji
kwa kuandika au kuzungumza vitu visivyo vya kweli COSOTA inakemea vikali tabia
hii,"alisema Doreen.
Pamoja na hayo Bi. Doreen
alifafanua kuwa COSOTA haijakusanya mirabaha kutoka katika Redio Saba tu kama
ilivyoelekezwa bali imekusanya kutoka vyanzo mbalimbali kama Baa, Hoteli, Kumbi
za Sherehe, Kumbi za Starehe na vyombo vya habari kama Kebo, Redio na
Televisheni.
Aidha, Mtendaji Mkuu huyo wa
COSOTA amefafanua kuhusu hoja ya fedha zilizopokelewa kutoka taasisi ya
Hakimiliki ya CAPASSO ya nchini Afrika ya Kusini, kiasi cha Milioni ishirini na
moja kupelekwa katika mfuko wa Sanaa na Utamaduni nikutokana na fedha
hizo kuwa na viwango vidogo kwa wanufaika ambapo mara baada ya kugawa wanufaika
walikuwa akipata kiasi cha Tshs. 2,214 na hapo zilihitajika kukatwa 5%.
Hivyo COSOTA inatoa wito kwa
wabunifu wote kuendelea kusajili kazi zao kwa ajili ya kuziwekea ulinzi, na
inasisitiza kuwa mgao wa mirabaha unatokana na matumizi ya kazi kibiashara na
siyo kwamba unaposajili tu kazi yako unakuwa unastahili kulipwa mrabaha.
********************MWISHO**********************