Diwani
wa Kilawani, Mussa Kafana (CUF), ameibuka mshindi wa nafasi ya Naibu
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, huku matokeo hayo yuakiwashangaza wengi
kwa kuwa idadi ya madiwani wa CCM walikuwa sawa na wale wanaounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mshangao
huo unatokana na hali ilivyotokea kinyume cha matarajio kwani kutokana
na idadi ya madiwani wa CCM na upinzani, wengi walidhani kuwa huenda
kura baina ya pande husika zingekuwa sawa. Katika uchaguzi huo, madiwani
wa CCM walikuwa 11 kama walivyo wa Ukawa.
Pamoja na matokeo hayo, Kafana alipata kura 12 na kumshinda mpinzani wake, Mariam Lulida (CCM) aliyepata kura 10.
Katika
uchaguzi huo ambao ulikuwa na mvutano wa muda mrefu kati ya Ukawa na
CCM, katika kikao cha Baraza la Jiji, mgombea huyo wa CUF ililazimika
kufikishwa ukumbini kushiriki kupiga kura licha ya kwamba ni mgonjwa.
Mvutano
ulianza kutokea baada ya Kafana kushindwa kufika kwa madai alikuwa
mgonjwa, hatua ambayo iliwafanya madiwani wa upinzani kugoma
kujiorodhesha mpaka mgombea wao afikishwe ukumbini kwa kuwa hawana
taarifa za kuumwa kwake.
Madiwani
wa CCM kwa upande wao walikuwa wanagoma diwani Kafana kuletwa ukumbini
kwa vile ni mgonjwa huku wapinzani wakidai kuna kuwa kuna mchezo ambao
unafanywa na CCM ili usifanyike uchaguzi kwa vile taarifa za kuumwa
hawazifahamu.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, aliingilia kati na kusisitiza kwamba mgombea huyo ni mgonjwa.
Licha
ya kutoa taarifa hiyo, hali haikuwa shwari na ndipo madiwani wa
upinzani walipotaka mgombea wao aletwe ukumbini hata kama ni mgonjwa na
hatimaye kufikishwa akiwa amebebwa kutokana na hali yake.
Baada ya kufikishwa ukumbini alilazwa kwenye kiti hali ambayo iliwashtua baadhi ya wajumbe wakajikuta wanamwonea huruma.
Meya
aliomba mwongozo wa kuahirishwa kwa kikao hicho kwa madai kuwa haikuwa
halali kwa mgonjwa kufikishwa ukumbini kwa kuwa hali yake si nzuri.
“Baada
ya kuona hali yake, naomba kikao hiki kiahirishwe, tukifanye siku
nyingine. Limefanyika kosa kubwa sana kumleta mtu huyu hapa na
menejimenti ifanye utaratibu wa kumpeleka hospitalini sasa hivi,”
alisema.
Meya
aliahirisha mkutano huo na mgonjwa kuamriwa kupelekwa hospitali, lakini
baada ya mgonjwa kutolewa nje ya ukumbi, Mkurugenzi wa Jiji alisimama
na kutaka kikao kiendelee na uchaguzi ufanyike kwa madai kwamba idadi
imetimia.
Kutokana
na kauli hiyo, madiwani wa Ukawa iliwalazimu kumbeba mgonjwa wao na
kumrudisha ukumbini na alisaidiwa kupiga kura na Mbunge wa Ubungo, Saeed
Kubenea, baada ya kikao hicho kuafiki.
Akimtangaza
mshindi huyo, Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, alisema wapigakura
walikuwa 22, kura zilizopigwa zilikuwa 22 na hakuna kura iliyoharibika.
Alisema
baada ya uchaguzi huo, Kafana alipata kura 12 na Lulida kura 10 ikiwa
ni tofauti ya kura mbili, hivyo kumtangaza Kafana kuwa mshindi wa kiti
hicho.
Baada
ya matokeo kutangazwa , mshindi huyo ambaye alikuwa hajiwezi kutembea,
alinyanyuka na kisha kutembea na kuingia katika gari lake.
CHANZO:MPEKUZI