PICHA:KUTOKA MAKTABA
Na.Shija Felician,Geita
Idadi kubwa ya wanafunzi katika
shule ya msingi Kasandalala wilayani Mbogwe mkoani Geita wanasomea nje
madirishani baada ya vyumba vya madarasa kujaa kutokana na msongamano mkubwa watoto
waliotokana na mpango wa serikali wa elimu bure.
Hali hiyo imeelezwa jana na
mtendaji wa kijiji cha Shinyanga B kata ya Nyakafulu wilayani Mbogwe Machibya
Elias wakati wa tathimini wa mradi wa utawala bora na uwajibikaji unaotekelezwa
na shirika Capacity Building
Initiatives for poverty alleviation CABUIPA ambapo amesema hali hiyo imesababisha
ufundishaji wa wanafunzi kuwa mgumu.
Elias
amesema kutokana na msongamano huo wanafunzi wa darasa la pili wanaoingia la
tatu wako mia saba na wale wa darasa la kwanza wanaoingia la pili wako mia tano
na wote wameandikishwa kwenye mpango wa serikali wa elimu bure ambapo kila
darasa wanasoma chumba kimoja na shule hiyo ina wanafunzi elfu tatu mia moja
themanini huku ikiwa na vyumba saba tu vya madarasa.
Naye
mwezeshaji wa utawala bora kutoka shirika la Capacity Building
Initiatives for poverty alleviation CABUIPA Michael Ikila amewataka viongozi wa
serikali katika kijiji hicho kila mmoja kutumia wajibu wake kwenye madaraka
aliyonayo kuonesha ushirikiano kumaliza tatizo hilo kutokana na maendeleo
huletwa na wananchi wenyewe.
Kwa
upande wake ofisa elimu wa wilaya ya Mbogwe Samwel Muyemba amesema tayari kuna
mkakati wa kumaliza tatizo hilo shuleni hapo kwa kuigawa mara mbili shule hiyo
pamoja na kupunguza wanafunzi kwa kuwapeleka shule jirani ingawa tayari kuna
ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa ambayo yatakamilika kabla ya wanafunzi
hawajafungua mwezi Januari.
Mwisho