Na Mwandishi wetu -DODOMA.
SERIKALI imewataka wadau wa elimu na jamii kwa ujumla kuendelea kuwahamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wataalamu wanawake na kuleta uwiano unaohitajika katika sekta hiyo muhimu kwa Maendeleo ya Taifa.
Hayo yamesemwa leo Februari 11, 2026 Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Prof. Adolf Mkenda wakati akizungumza katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, ambapo amesema takwimu zinaonesha kuwa wanawake wanasayansi duniani ni asilimia 36 pekee, hali inayoashiria kuwepo kwa pengo kubwa la kijinsia katika taaluma za sayansi.
Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, asilimia 51 ya Watanzania ni wanawake, jambo linaloonesha kuwa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya sayansi nchini.
Prof.Mkenda amesema ushiriki mkubwa wa wanawake katika sayansi utachangia kukuza ubunifu, tafiti na teknolojia zitakazosaidia Taifa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo.
"Umefika wakati kwa wanawake na wasichana kujitokeza kwa wingi kuwekeza na kushiriki kikamilifu katika masuala ya sayansi ili kupanua wigo wa maarifa na kuleta mabadiliko ya kimaendeleo nchini."amesema Prof Mkenda.
Amesema kuna umuhimu wa kuwahamasisha wasichana kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kupenda masomo ya sayansi ili kujenga kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa.
Aidha akizungumzia umuhimu wa sayansi katika sekta ya afya, Prof. Mkenda amesema sayansi imekuwa chachu ya kupunguza vifo vya watoto na kuimarisha maisha ya wananchi kwa ujumla kupitia maboresho ya huduma za tiba, kinga na tafiti za kitabibu.
Hata hivyo kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha malezi bora kwa mtoto wa kike, jambo linalotoa fursa kwa wasichana wengi zaidi kusoma masomo ya sayansi.
"Usawa wa kijinsia katika elimu ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo endelevu, akitoa wito kwa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuendelea kuwaunga mkono wasichana katika safari yao ya kielimu, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia."amesema.
Awali Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mabula Magangila, amesema sayansi ni suluhisho la changamoto za kidunia na kwamba mtoto wa kike akihamasishwa zaidi anaweza kufanya vizuri hata kuliko mtoto wa kiume.
"Serikali imeboresha mazingira ya elimu ya sayansi na kwamba Bunge litaendelea kutunga sera bora zitakazomuwezesha mtoto wa kike kupata haki sawa ya elimu, hususan katika masomo ya sayansi."amesema Mhe.Mabula.






