Na Mwandishi wetu - Dodoma.
CHUO cha Uhasibu Arusha(IAA) kimeendelea kuwaandaa vijana kwa kuweka mazingira Bora ya ya kujifunzia ili kuendana na soko la ajira pamoja na kujiajiri kwa kuwapatia elimu ya fedha na ujuzi wa biashara.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, wakati kizungumza na waandishi wa habari Februari 20, 2026 jijini Dodoma ambapo amesema chuo hicho kimejikita katika kuwaandaa vijana kwa kuwapatia elimu ya fedha na ujuzi wa biashara ili waweze kujiajiri na kujitegemea.
"Vijana wengi wana ujuzi wa kitaaluma na kiufundi, lakini wanakosa maarifa ya namna ya kuugeuza ujuzi huo kuwa fursa ya ajira na kuepukana na utegemezi."amesema.
Prof.Sedokeya amesema katika kuimarisha ajira kwa vijana, chuo kimeanzisha mtaala mpya wa uhasibu na kodi unaolenga kumwezesha kijana kujiajiri pamoja na elimu ya fedha na nidhamu ya matumizi, ikiwemo namna ya kupata fedha kupitia maandiko yao ya biashara.
Amesema wahitimu wanaweza kusaidia kuandaa hesabu, kuziweka vizuri na kutengeneza taarifa za kodi ambapo mtaala wa Accountancy International unawaunganisha vijana na ujuzi na weledi unaowawezesha kuingia kwenye soko la ajira au kujiajiri.
Aidha,Prof.Sedokeya amesema kozi zinazotolewa zimeandaliwa kwa kuzingatia uhalisia wa mahitaji ya vijana na soko la ajira, na chuo kina ushirikiano na Jeshi la Magereza katika kuwapatia vijana walioko gerezani na wanaokaribia kutoka mafunzo ya elimu ya fedha na ujuzi wa kujiajiri, ili wanapotoka waweze kuanza shughuli halali na kuepuka kurejea tena gerezani.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo hutolewa kidigitali kutoka chuoni hadi gerezani na chuo kina jumla ya wanafunzi 20,993 katika kampasi zake mbalimbali, huku takribani wanafunzi 1,000 wakiwa siyo active kutokana na changamoto mbalimbali.
Hata hivyo,Prof. Sedoyeka amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika chuo hicho kwa lengo la kuwafikia wananchi zaidi, huku asilimia 90 ya wanafunzi wakiwa vijana wa wastani wa umri wa miaka 20.



