SERIKALI YATANGAZA KUFUTA LESENI 73 ZA WACHIMBAJI WA MADINI.

MUUNGANO   MEDIA
0


 

Na Avelina Musa - Dodoma .

Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde ameiagiza Tume ya Madini kufuta jumla ya leseni 73 ambazo wamiliki wake wameshindwa kuziendeleza pamoja na kushindwa kurekebisha makosa yaliyobainishwa katika ukaguzi wa hivi karibuni.


Mhe.Mavunde amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 25,2025 Jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya msimamo wa serikali kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya Taifa.





" Sitawavumilia watu wanaochukua leseni na kukaa nazo bila kuziendeleza,Naiagiza Tume ya Madini kufuta jumla ya leseni 73 ambazo wamiliki wake wameshindwa kurekebisha makosa" amesema Mhe.Mavunde.

Mhe.Mavunde amesema Tume ya Madini ilitoa Hati za Makosa kwa leseni 205, ikijumuisha leseni 110 za utafiti wa madini na leseni 95 za uchimbaji mkubwa na wa kati ambapo walitakiwa kurekebisha dosari hizo.

Amesema wamiliki wa leseni hizo wamekuwa wakikiuka masharti muhimu ya kisheria, ikiwemo kutowasilisha mipango ya maendeleo ya mradi, kushindwa kutekeleza masharti ya kifedha, kutoanzisha shughuli za utafiti au uchimbaji, na kuhodhi maeneo bila sababu za msingi.

Waziri Mavunde amewataka wamiliki wote wa leseni za madini kuhakikisha wanazingatia masharti na wajibu wa umiliki wa leseni zao, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote anayekiuka sheria.

"Nawaalika wawekezaji wenye nia ya dhati—wadogo kwa wakubwa—kuwasilisha maombi ya leseni katika maeneo ya wazi na  Wizara itaharakisha mchakato wa upatikanaji wa leseni kwa wakati."amesema.

Aidha Mhe.Mavunde ametoa wito kwa wawekezaji wote kutekeleza matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, huku Wizara ikiendelea kutoa ushirikiano kwa wote wanaotaka kufanya uwekezaji wenye tija katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)