Na Avelina Musa - Dodoma.
KATIKA kuhakikisha wakulima wanalima kwa Tija Kampuni ya Mrutu Agro Solutions imekuja na njia mbadala ya mifumo ya umwagiliaji ambayo wanawafungia wateja na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao kwa kuwapimia udongo wakulima ili waweze kujua virutubisho ambavyo vinahitajika katika kufanya kilimo cha mazao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mrutu Agro Solutions Limited Bwana philipo Fahamuel Mrutu wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kampuni hiyo imeamua kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Amesema utaalamu na uzoefu wake kuwasaidia wakulima hasa wadogo, kuboresha shughuli zao za kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi na kuongeza kipato chao.
Amesema kampuni ya Mrutu Agro Solutions wanatoa huduma mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa miche ya matunda kama vile miche ya miembe,michungwa,ndimu, komamanga,strawberry, parachichi na miche mingine mbalimbali.
"Miche hii ni miche ambayo imethibitishwa na inafanya vizuri katika maeneo mbalimbali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na ikiwa na sifa ya kutoa matunda na matokeo chanya ndani ya muda mfupi"Amesema.
Amesema Kampuni hii inajihusisha na uzalishaji wa mbolea hai ambayo inafanya vizuri sana katika kurutubisha afya ya udongo na kuboresha uzalishaji katika mazao, sambamba na hilo wapo na teknolojia ya vitalu nyumba kwa maana ya green house na (solar dryer) ambayo inatumia sola na gesi na inaweza kupunguza upotevu wa mazao kwa zaidi ya asilimia 40,
"Tuna mbegu za samaki bora kabisa aina ya sato na kambare mbegu ambazo zinalenga kuwapa fursa wafugaji wa samaki wanaohitaji kunufaika na fursa ya ufugaji wa samaki sababu sasa samaki ni biashara kubwa,kilo moja ni zaidi ya elfu 12 kwahiyo tunawapa huduma watu wanaotaka kujenga mabwawa ya samaki,wanaotaka mbegu za samaki lakini pia tunawapa ushauri waweze kufanikiwa." ameeleza Bwana Mrutu
Mrutu ameendelea kueleza kuwa kwa upande wa ufugaji kampuni yao inatoa huduma ya mbegu bora ya majani ya malisho na kutoa huduma ya kupanda majani ya malisho sambamba na huduma ya kujenga miundombinu bora ya ufugaji wa mifugo na wakiwa na mbegu bora za ng'ombe,Nguruwe, mbuzi na kadhalka.
Aidha Kampuni hii inawainua wakulima kupitia jukwaa la Agrisave ambalo linalenga kuwasaidia wakulima wadogo wasio na uwezo wa kununua pembejeo kwa gharama za mara moja kuweza kulipia pembejeo kidogokidogo ili msimu ukifika waweze kupata pembejeo bila riba kubwa kama vile mikopo ya kausha damu na kausha roho.
Mwisho.