Na Avelina Musa - Dodoma.
TUME huru ya Taifa ya uchaguzi ( INEC) imesema kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 28.2025 hadi Oktoba 28.2025 kwa Tanzania Bara na kuanzia tarehe 28 Agosti 2025 hadi tarehe 27 Oktoba, 2025 kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Kipindi cha kampeni, hutumiwa na mgombea, chama cha siasa au mwanachama aliyeidhinishwa kunadi wagombea, kuelezea sera na ilani za uchaguzi ili wananchi waweze kufanya maamuzi tarehe itakapofika.
Hayo yamesemwa Leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele katika Mkutano wa Kitaifa wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na Vyama vya siasa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,Wenye kauli mbiu "Kura Yako Haki yako Jitokeze Kupiga Kura".
Mhe.Jaji Mwambegele amesema Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi inawahakikishia kuwepo kwa uwanja sawa kwa vyama vyote wakati wa kampeni kwa kuhakikisha kila chama kitafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba itakayokuwa imepitishwa na kamati ya ratiba ngazi ya Taifa inayoratibu ratiba ya kampeni ya wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais.
"Na kamati ya jimbo inayoratibu ratiba ya wagombea wa ubunge na kamati ya kata
inayoratibu ratiba ya wagombe wa udiwani"amesema Mhe.Jaji Mwambegele.
Aidha,Mhe.Jaji Mwambegele amewaasa vyama vya siasa pamoja na wafuasi wao kufanya kampeni za kistaarabu na hivyo kuepuka kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi yetu.
"Majimbo yatakayotumika kwenye uchaguzi ni 272 ambapo majimbo 222 yapo Tanzania Bara na Majimbo 50 yapo Tanzania Zanzibar na Idadi hii ya majimbo ya uchaguzi kuna ongezeko la majimbo nane (08)yaliyoanzishwa
kwa upande wa Tanzania Bara"Amesema.
Amesema jumla ya Kata 3,960 zitafanya uchaguzi wa Madiwani, idadi hii ni ongezeko la kata tano (05) zilizoongeka baada ya Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzisha kata mpya Tano.
Mhe.Jaji Mwambegele amesema Tume tayari imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa taasisi na asasi
164. Vilevile, Tume ilitoa mwaliko kwa taasisi na asasi za ndani na nje ya nchi zenye nia ya kuwa waangalizi wa Uchaguzi kuleta maombi na baada ya mchakato wa uhakiki, jumla ya taasisi na asasi 76 za ndani na 12 za kimataifa zimepata kibali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof.Ibrahim Lipumba ameipongeza Tume kwa Uwazi na ushirikiano wake kwa vyama vya siasa ambapo pamoja na pongezi hizo ameiomba Tume kuwaasa wasimamizi kutimiza wajibu wao kwa weledi bila upendeleo.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Addo Shaibu ameipongeza Tume kwa kufanya uboreshaji wa Daftari la kudumu la mpiga kura na ameiomba Tume kutoruhusu makada wa vyama vya siasa wasiwe sehemu ya wasimamizi wa Uchaguzi.
"Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kipekee sana kuliko miaka ya nyuma kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi".Amesema Addo.







