Na. Avelina Musa - Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za mitaa kutoa elimu ya kina kwa wakulima juu ya vipimo na matumizi sahihi ya mbolea ya FOMI katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Amesema inawezekana wakulima wakafikiwa na mbolea hiyo lakini wasiwe na maelekezo sahihi ya namna ya kuitumia ili kuhakikisha mbolea inatumika kwa tija na kwa kuzingatia viwango vinavyofaa kwa kila aina ya zao na ardhi husika.
Rais Dkt.Samia amesema hayo leo Juni 28,2025 Jijini Dodoma wakati akizindua Kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM kilichopo Nala, Jijini Dodoma.
Dkt.Samia ameutaka uongozi wa kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM kuhakikisha wanaimarisha mfumo wa usambazaji wa mbolea ili iweze kuwafikia wakulima waliopo vijijini.
“Nitoe rai kwa uongozi wa kiwanda cha ITRACOM kuhakikisha kwamba mnaimarisha mfumo wa usambazaji wa mbolea hadi kwa wakulima waliopo vijijini ili waweze kuipata mbolea hiyo kwa gharama nafuu na kwa wakati”amesema Rais Samia.
Hata hivyo ameongeza kuwa kwa kutoa elimu hiyo,kiwanda hicho kitakuwa kimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama wa chakula,kupunguza umasikini na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.
“Kiwango cha biashara kati ya Burundi na Tanzania kinaendelea kukua hivyo uwekezaji huu unaongeza fursa za ajira kwa vijana wetu, na kupitia mpango wa kuongeza vituo vya uuzaji wa pembejeo, wakulima sasa wanapata vifaa kwa gharama nafuu. Serikali imeanzisha pia mpango mkakati wa kujenga mabwawa ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa mvua.”
Pia Rais Samia amesema kuwa wameendelea kuonyesha jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya kilimo kwa kuwahakikishia wawekezaji wanakuwa na ushirikiano wa karibu.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Meja Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye,amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni hatua muhimu ya kuchochea maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akiwa ameambatana na mwenyeji wake,Rais Samia Suluhu Hassan,
Rais Ndayishimiye,amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa ya mahusiano kati ya Burundi na Tanzania.”Zamani tulikuwa tunakuja kama wakimbizi,sasa tunakuja kama wawekezaji.
“Naishukuru Serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa moyo wa ukarimu na kwa kuunga mkono mradi huo mkubwa,amefafanua kuwa kiwanda cha ITRACOM hakitachochea tu maendeleo ya kilimo bali pia kitaimarisha mshikamano wa kikanda”amesema Rais Ndayishimiye
Kwa Upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe,Hussein Bashe, ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa juhudi zake katika sekta ya kilimo.
“Serikali ya awamu ya sita imetekeleza kwa kina zana ya maendeleo kupitia wizara ya kilimo. Milioni 700 zimetengwa kwa ajili ya kuwapa wananchi ruzuku ya mbolea, na zaidi ya bilioni 500 zimetumika kwa ajili ya kuwapa wakulima wa korosho.
"Tanzania kwa sasa tunazihudumia nchi za Kenya, Congo, Kuanzia tarehe 1 Septemba 2025, wananchi wataanza kununua mbolea kwa bei ya ruzuku.” amesema Mhe.Bashe.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha ITRACOM Bw.Nduwimana Nazaire,amesema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mbolea Tani Milioni moja kwa mwaka huku ajira zaidi 1800 za moja kwa moja tayari zimeshatolewa.
“Ilikuwa kama ndoto, leo tumetimiza Ujenzi na kufungua kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha mbolea tani milioni moja kwa mwaka. Mwaka 2020 mradi ulianza kutekelezwa, wewe ukiwa kama Makamu wa Rais. Kwa msimamo wako dhabiti ulihakikisha kiwanda hiki kinatekelezwa na kujengwa.”amesema Bw.Nazaire.
Bw.Nazaire amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Burundi kwa kuruhusu uwekezaji huo wa mbolea hizo zinaboresha afya za udongo na zinaongeza mavuno, zimetengenezwa kwa mchanganyiko wa vitu mbalimbali.
“Kiwanda hiki kimetengeneza zaidi ya ajira 1,800 na kuna ajira zingine zisizo za moja kwa moja ambazo ni 3,000. Nipende kumshukuru Waziri wa Kilimo Mhe,Hussein Bashe, kwa usimamizi wake wa wizara. Tuna aina 14 za mbolea leo hii tarehe 28 Juni 2025. Mwaka 2021 tuliweza kuanza mradi kwa uwekezaji wa kujenga kiwanda hiki.”amesema.