Na Avelina Musa - Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson ameongoza zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Bunge, inayojengwa katika eneo la Kikombo, Jijini Dodoma.
Dkt.Tulia amesema hatua hiyo inatokana na maono ya muda mrefu ya kuwa na shule ya pekee itakayolea viongozi wa kesho kwa misingi ya maadili, nidhamu, na uzalendo, ikiwemo kukuza elimu ya kisayansi na uongozi bora miongoni mwa Wavulana.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Tulia amesema mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya pamoja wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwekeza kwenye elimu bora na ya maadili kwa vizazi vijavyo, bila kujali jiografia ya majimbo yao.
Amesema Ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya elimu Jijini Dodoma pamoja na kuongeza nafasi za wavulana kupata mazingira bora ya kujifunza, kuishi, na kukuza vipaji vyao kitaaluma na kijamii.
“Tunawashukuru sana wabunge na wadau wote waliotuunga mkono katika hatua ya awali,tunawaomba waendelee kushirikiana nasi kwa kuchangia fedha, vifaa vya ujenzi, au hata ushauri wa kitaalamu,” amesema.
“Fedha za awali zilizowezesha kuanza kwa ujenzi huu ni mchango wa waheshimiwa wabunge kupitia posho zao,Wamechangia kwa moyo mmoja, bila kuangalia kwamba shule inajengwa Dodoma,”amesema Dkt.Tulia.
Amesema sehemu nyingine ya fedha na vifaa ni mchango wa wadau mbalimbali waliokuwa wakishiriki katika matukio kama Bunge Bonanza pamoja na marafiki wa maendeleo walioguswa na dhamira hiyo ya kitaifa.
Dkt. Tulia amesema Taasisi hiyo ya elimu italeta manufaa ya muda mrefu kwa taifa, kwani itakuwa chimbuko la viongozi, wataalamu, na wajasiriamali watakaolijenga taifa katika karne ya sasa na zinazokuja.
Aidha Dkt.Tulia amewataka wananchi, Taasisi binafsi, mashirika ya umma na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kuunga mkono ujenzi wa shule hiyo kama sehemu ya jukumu la pamoja la kuimarisha elimu nchini.