NCAA YASEMA IMEFANIKIWA KUBORESHA UHIFADHI WA WANYAMAPORI NA KUONGEZA IDADI YA WATALII KATIKA MIAKA MINNE YA DKT.SAMIA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.


Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, wamefanikiwa kuboresha uhifadhi wa wanyamapori, kuongeza idadi ya watalii na mapato pamoja na kuboresha maisha ya wenyeji na kuboresha miundombinu ya utalii. 


Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Dkt. Elirehema Doriye leo Machi 10, 2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.


Dkt. Doriye amesema, katika mwaka wa fedha 2024/25 kuanzia mwezi Julai hadi Februari 2025, tayari NCAA imeshakusanya shilingi bilioni 212 huku idadi ya watalii ikifikia 830,295 inayojumuisha watalii wa nje 509,610 na watalii wa ndani 320,685, mwenendo unaonyesha mamlaka itapata watalii zaidi ya milioni moja na mapato zaidi ya lengo ambalo ilijiwekea la kukusanya shilingi bilioni 230 kwani hadi sasa katika mapato haya, imeshakusanya asilimia 92.


"NCAA inatarajia kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2024/25 la kukusanya shilingi bilioni 230 kwani hadi kufikia Februari 2025, tayari imeshakusanya asilimia 92 ya mapato hayo"Alisema Dkt. Doriye.



Ameongeza kuwa, takwimu zinaonesha kati ya Julai 2021 hadi Februari 2025, jumla ya watalii 2,916,540 wametembelea vivutio vya utalii ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na katika kipindi hicho, mapato ya shilingi bilioni 694 yamekusanywa na kuingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.


Dkt.Doriye amesema, takwimu hizo zinaonesha kuwa juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania zimechangia kutangaza nchi na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya utalii. Vilevile, mikakati mbalimbali ya shirika pamoja na ushirikiano kati ya sekta binafsi na mamlaka za utalii umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo.


Aidha, ameitaja mikakati mbalimbali ya mamlaka hiyo ya kutangaza utalii ikiwemo kwenye matumizi ya teknolojia ya kidijitali, ushirikiano na wadau wa utalii, kampeni za kijamii na utalii wa ndani, matumizi ya Wanahabari na Waandishi wa Habari, uanzishaji na matumizi ya matukio maalum pamoja na ununuzi wa basi jipya lenye uwezo wa kubeba abiria 40. 


Katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, NCAA imefanikiwa kuboresha uhifadhi wa wanyamapori, kuongeza idadi ya watalii na mapato, kuboresha maisha ya wenyeji na kuboresha miundombinu ya utalii. Mamlaka itaendelea kuhakikisha Ngorongoro inabaki kuwa kivutio bora cha utalii duniani kwa kulinda rasilimali za asili na utamaduni kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)