KUELEKEA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA FCC YAWAKUMBUSHA WATANZANIA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA MPIGA KURA.

MUUNGANO   MEDIA
0


Na Avelina Musa - Dodoma.

 Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio amewakumbusha Watanzania kujiandikisha kwenye daftari la Mpiga kura ili kupata nafasi ya kuwachagua Viongozi wenye maono na fursa zinazowahusu.

Erio amesema hayo leo Agosti 5,2024 kwenye Maonesho ya wakulima yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya Nanenane-Nzuguni Jijini hapa na kueleza kuwa Viongozi hao wanapaswa kuwa na uelewa mzuri wa mahitaji ya wafanyabiashara na sera zinazohitajika ili kuboresha kilimo na fursa zake

Amesema kuwa Viongozi bora ni wale wenye mipango thabiti na mikakati ya maendeleo ya kilimo na kuweza kujumuisha mipango ya kuboresha miundombinu, masoko, na upatikanaji wa huduma za kilimo.

"Niwaombe wafanyabiashara mchague viongozi wenye uwezo wa Kuleta mabadiliko Viongozi wenye mtandao mzuri na uhusiano na wanaweza kusaidia kufanikisha ushirikiano wa kibiashara, kupata ruzuku, na rasilimali nyingine za maendeleo,viongozi wanapaswa kuwa na uwezo wa kusimamia na kuboresha huduma za kibiashara na kilimo kwa kujumuisha usimamizi wa ardhi, maji, na miundombinu ya kilimo, "amesema

Amesema Tume ya Ushindani, ambayo ndiyo inashughulikia masuala ya ushindani wa kibiashara, ina jukumu muhimu la kutoa ushauri kwa kampuni zinazoshindana katika soko ikiwemo kujitambulisha kwa Soko,kulijua soko vizuri na mahitaji ya wateja.

" FCC tunajukumu la kuhakikisha mfanya biashara anatambua nafasi yake katika soko ili kuboresha bidhaa na upekee,ili kuwa na tija mfanyabiashara anapaswa kujitofautisha kupitia bidhaa , tafuta njia za kutofautisha bidhaa zako zile za washindani hii itaboresha ubora, kuongeza vipengele vya kipekee, au kutoa huduma bora kwa wateja,"amesisitiza

Aidha Erio ameongeza kuwa kila mfanyabiashara anapaswa kuhakikisha bidhaa zake zinakidhi viwango vya ubora vinavyotambulika na vya kisheria na kufafanua kuwa ubora wa bidhaa unaweza kuwa kipande muhimu katika ushindani.

" Jenga jina la bidhaa yako kwa kusikiliza maoni ya wateja kunaweza kusaidia kuboresha bidhaa na huduma zako, Maoni ya wateja yanaweza kutoa mwanga kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa lakini pia hakikisheni mnatafiti masoko kubaini mwelekeo na mahitaji mapya, "amesema Erio.

Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)