WAZIRI MKUU AAGIZA KUWEKWA MKAKATI WA KUONGEZA VIRUTUBISHI KATIKA CHAKULA
Author -
MUUNGANO MEDIA
Jumamosi, Juni 15, 2024
0
Na WAF - DSM
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka
Wizara mtambuka za Afya, TAMISEMI pamoja na Viwanda na Biashara kuweka
mkakati wa kuongeza virutubisho katika chakula ili kukabiliana na
magonjwa yanayotokana na lishe duni katika jamii.
Mhe. Kassim
Majaliwa amesema hayo leo jijini Dar Es Salaam wakati akizindua kiwanda
cha kutengeneza viturubishi (Premix Blending Plant) cha Kampuni ya SANKU
- PHC Tanzania. Mhe. Majaliwa amesema suala la lishe ni mtambuka
hivyo linahitaji nguvu ya pamoja ili kuweza kukabiliana na lishe duni
hasa katika maeneo ambayo yana udumavu kwa watoto na ukosefu wa damu
hivyo Wizara kwa kushirikiana na wadau zinatakiwa kutengeneza mpango wa
kufikisha bidhaa zenye virutubisho ikiwemo unga wa mahindi, unga wa
ngano na mafuta ya kupikia.
"Katika kuhakikisha hili
linafanikiwa, Serikali katika awamu zote imekua ikishirikiana na Wadau
mbalimbali imekua ikitengeneza mpango mkakati wa lishe kwa kuongeza
virutubishi ambavyo vinasaidia kuupa mwili lishe ikiwemo kuweka madini
joto kwenye chumvi, madini chuma na folic acid kwa watoto na wanawake
wajawazito ili kuounguza tatizo la upungufu wa damu na uzito mdogo".
Amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wamiliki wa
kiwanda cha SANKU kwa kuwekeza nchini katika eneo hilo la kuongeza
virutubishi ambapo itasaidia kuondokana na gharama zilizokua zinatumika
kuagiza virutubishi hivyo kutoka nje ya nchi ikiwemo malighafi, kwani
kiwanda hicho sasa kitakua kinatumia malighafi zinazopatikana hapa
nchini. Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Afya Mhe. Ummy
Mwalimu amesema takwimu za lishe zilizotolewa mwaka 2022 zinaonesha
kuwa kwenye kila watoto kumi wenye umri chini ya miaka mitano Tanzania
watatu kati yao wana tatizo la udumavu ikiwa ni sawa ni watoto milioni
tatu nchi nzima.
Kufuatia hali hiyo Waziri Ummy amesema Serikali
kwa kushirikiana na Wadau imeweka mikakati ya kukabiliana na udumavu kwa
kuboresha hali ya lishe nchini hivyo uwepo wa kiwanda hicho kutasaidia
katika kukamilisha mikakati hiyo.