Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Mei 26, 2024 amewasili Geneva nchini Uswisi akiongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao cha juu 77 cha maamuzi kuhusu masuala ya Sekta ya Afya Duniani ya Shirika la Afya (WHO).
Baada ya kuwasili, Waziri Ummy amekaribishwa katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Geneva na kupokea taarifa ya maandalizi ya kikao hicho kutoka kwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania wa Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi Dkt. Abdallah Possi.
Waziri Ummy ameongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho akiambatana na Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu pamoja na wataalam wengine kutoka ubalozini na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Mkutano huo huwashirikisha Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa WHO ambapo katika mkutano huo wa 77 wa Shirika la Afya Duniani utakuwa na agenda kuu Tano ikiwemo marekebisho ya Sheria ya Afya ya Kimataifa, majadiliano ya mkataba wa Kimataifa wa kujikinga, Kuzuia na utayari wa kupambana na majanga ya Afya.
Ajenda nyingine ni pamoja na mpango mkakati wa Kumi na Nne wa Shirika la Afya Duniani utajadiliwa, mkakati wa ugharimiaji na uwekezaji katika Sekta ya Afya pamoja na maazimio Kumi ya uimarishaji wa huduma na mifumo ya Afya Duniani.
Wakati wa kikao hicho Waziri Ummy na Waziri Mazurui watashiriki kwenye mikutano ya pembeni ya masuala mahususi ya Afya sambamba na kufanya kampeni za kumnadi Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) ambaye anagombea nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika (WHO AFRO).