Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya habari,Mhe,Nape Nnauye ameipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL) kwa kufanikiwa kukusanya shilingi 135,216,317,693 hadi kufikia Aprili 2024 katika mwaka wa fedha 2023/24 sawa na asilimia 56.34 ya lengo lililopangwa la kukusanya Shilingi 240,000,000,000 kutokana na huduma za mawasiliano, ukodishaji wa vifaa vya mawasiliano, upangishaji majengo na ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Waziri Nape ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Mhe,Nape amesema hadi kufikia Aprili 2024 shirika hilo lilifanikiwa kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 22 za Karatu, Mbulu, Longido, Hai, Mwanga, Pangani, Muheza, Lushoto, Kibiti, Mtama, Nachingwea, Newala, Mbinga, Ludewa, Ileje, Vwawa, Mbogwe, Msalala,Tarime, Sengerema, Rorya na Ngara.
Aidha amesema TTCL imefanikiwa kuunganisha watumiaji 12,584 wa huduma za faiba mlangoni sawa na asilimia 63 ya lengo.
"Shirika limefanikiwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya Wi-Fi katika maeneo manne ya umma ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo
cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Uwanja wa Benjamin
Mkapa Jijini Dar es Salaam,"alisema Nape.
Aidha Waziri Nape amesema kuwa TTCL ilifanikiwa kufanya tafiti mbili za kuridhika kwa wateja ambapo lilisajili wateja 102,850 wapya wa T-PESA
kwa ajili ya kutumia huduma za kifedha za T-PESA na Kuunganisha Taasisi sita za Serikali na Binafsi kwa ajili ya huduma za malipo ya mkupuo (bulk disbursement).
Waziri Nape ameeleza kuwa shirika hilo lilifanikisha kusainiwa kwa Mikataba ya mauzo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi za Uganda wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 28.8, Malawi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5 na Kampuni ya Airtel wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.8.
Mwisho