TANZANIA YAPONGEZWA KUANZISHA MPANGO JUMUISHI WA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII
Author -
MUUNGANO MEDIA
Jumatano, Mei 29, 2024
0
Na WAF - Geneva, Uswisi
Wadau
wa maendeleo katika Sekta ya Afya waipongeza Tanzania kwa kuanzisha
mpango jumuishi na shirikishi wa wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii
utakaowafikishia wananchi huduma za Kinga, Tiba na Elimu ya Afya mahali
walipo bila vikwazo vyovyote.
Wadau hao wameipongeza Tanzania
baada ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kuwaeleza umuhimu wa kuwatumia
wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) ikiwa ni mkakati wa kuimarisha
utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi na kufikia lengo la Afya kwa
wote. Waziri @ummymwalimu
amesema hayo Mei 28, 2024 kwenye Mkutano uliofanyika pembezoni mwa
Mkutano Mkuu wa 77 wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unaoendelea Jijini
Geneva nchini Uswisi uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa
mashirika ya Umoja wa Mataifa, Taasisi za Kimataifa pamoja na mashirika
yasiyo ya Kiserikali ya ndani na nje ya nchi.
"Wadau hawa pia
wameahidi kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mpango
utakaoleta mabadiliko na kuboresha Afya za wananchi ikiwemo kutoa
rasilimali watu na fedha kwa kuendelea kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi
ya Jamii." Amesema Waziri Ummy Katika mkutano huo pia
uliambatana na mdahalo wa wataalam wabobezi wa Afya ngazi ya msingi
kutoka ndani na nje ya nchi ambao walieleza kwa kina na kwa ushahidi
namna mpango huo utakavyoleta mabadiliko na kuboresha Afya za wananchi.
Kwa
upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema Serikali
imejipanga kutekeleza mpango huo katika Mikoa yote 26 na Halmashauri
184 za Tanzania lengo likiwa ni kufikia vijiji vyote 12,318, Mitaa 4,263
na vitongoji 64,384 kwa kuwa na watoa huduma za Afya ngazi ya Jamii
wawili wawili na hivyo kuwa na jumla ya wahudumu laki 137,294. Mkutano
huo ambao uhudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 wakiwemo Mawaziri wa
Afya kutoka nchi za Afrika na mabara mengine, umedhihirisha wazi
matarajio na mategemeo ya wadau kuwa mpango huo utakuwa wa mfano katika
kuboresha uratibu wa afua mbalimbali za Afya zinazotekelezwa na Serikali
kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.