
Idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka hadi 520,324 katika kipindi cha januari hadi machi 2024,ikilinganishwa na watalii 409,082 walioingia nchini katika kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la watalii 111,242 sawa na asilimia 27.
Hayo yameelezwa na Daniel Masolwa Mkurugenzi wa takwimu za uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa viashiria vya kiuchumi vya muda mfupi kwa kipindi cha mwezi januari hadi marchi 2024.
Masolwa amesema idadi ya watalii walioingia nchini mwezi machi 2024 iliongezeka hadi 155,810 ikilinganishwa na watalii 118,186 walioingia nchini mwezi machi 2023 ikiwa ni ongezeko la watalii 37,624 sawa na asilimia 31.8
Amesema idadi kubwa ya watalii walioingia nchini kutoka nje ya bara la afrika walitoka Italia,ufaransa na marekani,wakati idadi kubwa ya watalii kutoka katika Bara la afrika walitoka Burundi,Kenya na Zambi.
Aidha Masolwa ameongeza kuwa huduma ya mawasiliano imekuwa ni kichocheo kikubwa cha shughuli mbalimbali za kiuchumi Tanzania na dunia kwa ujumla, ambapo katika kipindi cha januari hadi machi 2024 huduma ya mawasiliano iliendelea kuongezeka hadi dakika za kuongea bilioni 34.96 kutoka dakika bilioni 32.04 kipindi kama hicho mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la dakika bilioni 2.93 sawa na asilimia 9.1
Sanjari na hayo amesema kuwa kiasi cha mvua za wastani ni mihimu katika ukuaji na mchango wa shughuli za kilimo katika pato la taifa na pia kuwezesha upatikanaji wa chakula kwa wananchi na baadhi ya malighafi za viwandani.
"Mwenendo wa kiasi cha mvua kilichopatikana nchini katika kipindi cha januari hadi machi 2024 kilifikia milimita 15,393.2 ikilinganishwa na milimita 10,396.1 mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la milimita 4,997.1 sawa na asilimia 48.1 "Alisema.
Mwisho.