MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAANZA RASMI- DKT. BITEKO
Alhamisi, Machi 07, 2024
0
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesemakuwa safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza rasmi
nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa
wananchi na hasa kina mama Tanzania wanahama kutoka matumizi ya
nishati ya kupikia isiyo safi kwenda kwenye nishati iliyo safi na
salama.
Amesema hayo tarehe 7 Machi, 2024 wilayani Temeke Mkoa wa Dar es
Salaam wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi na majiko banifu kwa
wajasiriamali katika Soko la Temeke Stereo na Mbagala- Zakhem.
“Nataka niwaeleze kuwa, safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia
imeanza katika wiki hii ambayo tunasherehekea siku ya Wanawake Duniani
kwa sababu tunafahamu kwamba Mwanamke ni mwathirika mkubwa nishati
isiyo safi ya kupikia na wanapata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa
wa kifua, kubakwa na kutumia muda mrefu kutafuta kuni hivyo Serikali
imeona kuwa ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ili kumwezesha
mwanamke kupata nishati safi na kwa gharama nafuu.” Amesema Dkt.
Biteko
Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa
matumizi ya nishati safi ya kupikia siyo tu kwa Tanzania bali Afrika
nzima na ulimwenguni; na hii ilithibitika wakati akizindua Programu ya
Nishati safi ya kupikia itakayosaidia Wanawake Barani Afrika (African
Women Clean Cooking Support Programme (AWCCSP) katika Mkutano wa Cop
28 Dubai ambayo imeungwa mkono na wadau mbalimbali hivyo kama nchi
lazima iwe na mpango maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia.
Ameongeza kuwa, zoezi hilo la ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko
banifu halitaishia Dar es Salaam bali ni endelevu na litafanyika
katika mikoa mbalimbali nchini ili wananchi katika maeneo yote
wahamasike kutumia nishati safi ya kupikia.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wa Dini, Serikali,
Jadi na makundi mengine kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia huku
akisisitiza kuwa ajenda hiyo isiwe ya Serikali pekeyake, ambapo pia
ameomba wadau zaidi wajitokeze kuungana na Serikali katika suala hilo
kama ilivyo kwa kampuni ya Oryx ambayo imeonesha kwa vitendo kuwa
inaiunga mkono Serikali kwenye nishati safi ya kupikia.
Aidha, amezitaka Taasisi kama vile Shule, Magereza na Hospitali
watumie gesi kwenye matumizi ya kupikia na kuanza kubadilisha mifumo
ya matumizi ya kuni kwenda kwenye Gesi ili kufanikisha ajenda ya
Serikali ya Matumizi ya Nishati safi ya kupikia.
Dkt. Biteko pia amesisitiza utunzaji wa mazingira na misitu ili
kuweza kupata maji ya uhakika, umeme na masuala mengine yanayotokana
na utunzaji wa mazingira na kueleza kuwa ili vizazi vijavyo visiishi
kwenye jangwa ni lazima kuchukua hatua sasa za kuzuia uharibifu wa
mazingira.
Kutokana na hilo, ameagiza wasimamizi wa Misitu nchini ikiwemo
Halmashauri na Serikali za mitaa kujikita kwenye uhifadhi na utunzaji
wa mazingira badala ya kusubiri kukamata mkaa. Amesema kila mtu lazima
atimize wajibu wake, kuacha tamaa ya kupata fedha kidogo kwa gharama
ya mazingira na kwamba jambo la kulinda mazingira na misitu ni jambo
la lazima.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, hali ya upatikanaji
umeme nchini ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam inaendelea kuimarika na
kwamba kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuna changamoto ya miundombinu ya
kusafrisha umeme lakini Serikali inatenga fedha za kuimarisha
miundombinu hiyo ambapo laini ya umeme kutoka Gongolamboto kwenda
Mbagala inaimarishwa kwa kujenga laini kubwa zaidi ya umeme na pia
transfoma iliyopo Mbagala yenye ukubwa wa MVA 50 inabadilishwa na
kuwekwa ya MVA 120.
Amesema pia inajengwa laini ya umeme chini ya ardhi ya kilometa 6
kutoka Kurasini kwenda Ilala ambayo itapunguza mzigo wa laini ya
Mbagala na hivyo kufanya upatikanaji umeme kuwa tulivu na himilivu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga
amemshukuru Dkt. Biteko kwa maono yake ya kuhuisha azma na maono ya
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia
nishati safi ya kupikia na pia kuendeleza kampeni ya matumizi ya
nishati safi ya kupikia nchini.
Amesema kuwa tukio la leo ni mwendelezo wa matukio yaliyopangwa
kutekelezwa na Wizara ya Nishati ambapo tarehe 9 Machi, 2024 Wizara ya
Nishati itaendesha kongamano kubwa la Wanawake takribani 4000 kutoka
Wilaya na Mikoa yote nchini ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake duniani pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia.
Mhe. Kapinga amesema kuwa, asimilia 63 ya wananchi nchini wanatumuia
kuni kwa ajili ya matumizi ya kupikia, asilimia 25 wanatumia mkaa na
asilimia takriban 5 wanatumia nishati mbadala kama Gesi hivyo bado
safari ni ndefu kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia na
kwamba azma ya Rais ya asilimia 80 ya Wananchi kutumia nishati safi ya
kupikia ifikapo mwaka 2033 itafikiwa.
Amesema ugawaji wa vitendea kazi hivyo ni mwanzo tu kwani zoezi hilo
litafanyika nchi nzima kadri rasilimali zitakavyopatikana kwani lengo
ni kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameishukuru Wizara ya
Nishati kwa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa
kugawa mitungi hiyo ya gesi ambayo ameeleza kuwa itasaidia kuondoa
ukataji wa miti hovyo, kulinda dunia pamoja na ikolojia iliyopo.
Pia, amepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Nishati kupitia
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambazo zimepelekea changamoto
ya umeme kupungua kwa asilimia 85 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa
Dar es Salaam ikiwemo Mbagala.
Kwa upande wake, Katibu wa Mama Lishe, Soko la Temeke Stereo,
Mwanahamisi Nditi ameshukuru Serikali kwa kupata mitungi ya gesi na
majiko banifu ambayo itawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi kwenye
soko hilo na kueleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa na
changamoto kwao kutokana na kufanya kazi kwenye moshi mwingi ambao
unaathiri afya zao.
Pia ameomba kuwa zoezi hilo liendelee kutokana na uwingi wa mama lishe
katika soko hilo ambao ni takriban 78 na wasaidizi wao wapatao 70.
Viongozi wengine waliofuatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati katika hafla hiyo ya ugawaji wa mitungi ya gesi ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Naibu Katibu
Mkuu, Dkt. James Mataragio.
Caps
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akigawa
mitungi ya gesi kwa Wajasiriamali katika eneo la Mbagala jijini Dar es
Salaam ikiwa ni uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.