Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip
Mpango ameigiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na uongozi
wa mkoa wa Tanga kuchukua hatua za mapema katika kukabiliana na
changamoto ya soko la matunda yanayozalishwa mkoani humo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa
Kabuku Wilaya ya Handeni akiwa ziarani mkoani Tanga leo tarehe 21 Februari
2024. Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Tanga kufanya tathimini na kutambua
kiasi cha matunda yanayozalishwa katika eneo hilo.
Aidha Makamu wa Rais amemuagiza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara
kukutana na wamiliki wakubwa wa viwanda vya kuchakata matunda
(Bakhresa na Jambo Product) ili waweze kutumia matunda yanayozalishwa
Wilaya ya Handeni na Tanga kwa ujumla katika bidhaa zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kabuku na
Watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada katika utunzaji wa mazingira ili
kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Amesema athari za
uharibifu wa mazingira zimepelekea ongezeko la joto kupita kiasi, ongezeko la
mvua ambayo imepelekea uharibifu wa miundombinu na mlipuko wa
magonjwa.
Amesema ni muhimu watanzania kutambua uhifadhi ya mazingira ni jukumu
la kila mmoja kwa kuacha kukata miti ovyo, kuacha kuchoma misitu pamoja
na kupanda miti na kuitunza.
Makamu wa Rais amewasisitiza wananchi wa Kabuku kuhakikisha
wanazingatia elimu kwa watoto ili kuwa na kizazi bora na chenye maarifa kwa
manufaa ya Taifa. Pia amewaasa wananchi wa eneo hilo kuzingatia lishe kwa
kuwa ndio msingi wa afya bora ya mwili na akili.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Wizara imepokea shilingi bilioni 25
kwaajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji eneo la Segera hadi
Kabuku mkoani Tanga kwa lengo la kukabiliana na adha ya upatikanaji wa
maji katika eneo hilo. Waziri Aweso amesema mradi huo unatarajia kukamilika
mwanzoni mwa mwaka 2025 ambapo tayari mkandarasi anaendelea na kazi.
Aidha Waziri Aweso ametoa wito kwa mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi
na kukamilisha kwa wakati pamoja na kuwashirikisha wananchi na viongozi
wa eneo husika wakati wote wa ujenzi wa mradi huo. Aidha ameahidi kwamba
Wizara ya Maji itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama
ilivyopangwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa TAMISEMI Deogratius Ndejembi amesema
tayari Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) imepokea shilingi bilioni
30 ambazo zitaanza kushughulikia changamoto mbalimbali za barabara hapa
nchini. Ameongeza kwamba kwa upande wa Wilaya ya Handeni, Serikali tayari
imetenga fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Sindeni – Kwedikazo ya
kilometa 37.7 kwa kiwango cha lami. Amesema katika Wilaya hiyo TARURA
itaanza mchakato mara moja wa kuhakikisha barabara zilizoharibiwa na mvua
zinatengenezwa ili ziweze kupitika vema.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
21 Februari 2024
Tanga.

