MSITUMIE FEDHA TOFAUTI NA MAELEKEZO MLIOPATIWA- DKT. MAHERA

MUUNGANO   MEDIA
0

 OR-TAMISEMI.

Serikali imewataka Waratibu wa VVU/UKIMWI na Wahasibu wa  Halmashauri kutokutumia fedha za miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Global Fund kwa matumizi mengine tofauti ya maelekezo waliopatiwa na malengo kukusudiwa.


 Akizungumza leo  kwenye kikao kazi cha kujadili Takwimu na Matokeo ya Viashiria muhimu vya VVU/UKIMWI kupitia miradi inayofadhiliwa  mfuko huo kwa waratibu wa  UKIMWI na  Wahasibu wa Halmashauri kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Dkt. Charles Mahera, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya Dkt.Paul Chaote amesema kikao hicho  kitasaidia  kuwezesha na kuboresha hali ya utendaji katika Mikoa na wadau wanaoshirikiana  na Serikali.


 Amewataka maafisa hao kusimamia matumizi ya fedha zinazopelekwa katika maeneo yao zikiwa na lengo la kuboresha huduma za afya na kutekeleza shughuli mbalimbali za kutokomeza magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu, pamoja na ujenzi na kuboresha miundombinu inayolenga mazingira ya kutolea huduma za afya.

“Kumekuwepo na tatizo la baadhi ya Mikoa na Halmashauri kutowajibika ipasavyo katika usimamizi na ufuatiliaji wa uendeshaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuviacha vituo vikijiendesha wenyewe bila usimamizi na usaidizi wa kitaalamu unaohitajika kutoka  Timu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Huduma za Afya Ngazi ya Halmashauri (CHMT), sisi kama wasimamizi wa ngazi  ya Mikoa na Halmashauri ni jukumu letu kusimamia huduma za afya  na matumizi ya fedha tunazoletewa,”amesema.


Naye, Mhasibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Melton Nyella ametoa wito kwa maafisa kutokujifungia katika eneo moja na kuwahimiza kusimamia eneo la fedha.


Mratibu wa Mradi wa Global Fund kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI Dkt. Mwanahamis Hassan ametoa wito kwa maofisa hao kuwa wawazi wakati wa matumizi ya fedha na kuwasisitiza kuwa na takwimu sahihi za matumizi ya fedha wanazotumia na kuleta  taarifa mapema kwa ajili ya kuondoa hoja za kiukaguzi.





Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)