WAKAZI watatu wa Kigamboni jijinii Dar es
salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin
zenye uzito wa kilogramu 882.71 na Methamphetamine zenye uzito wa
kilogramu 2167.29.
Washitakiwa hao ni mfanyabiasha Najim Mohamed
(52) , mfanyabiasha Maryam Mohamed (50) na Juma Abbas (37) ambaye ni
msaidizi wa kazi za ndani.
Akisoma Mashtaka yao tarehe 29
Disemba, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Aaron Lyamuya, wakili wa
serikali mwandamizi Hemed Halfan ameniambia Mahakama kuwa, katika
shtaka la kwanza inadaiwa kuwa, Disemba 15, 2023 washtakiwa wote wakiwa
katika eneo la Kibugumo shule walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya
aina ya heroin zenye uzito wa kilogramu 882.71.
Katika shtaka la
pili alidai kuwa katika eneo hilo na siku hiyo washtakiwa hao walikutwa
wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa
kilogramu 2,167. 29.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka
yanayowakabili, hakimu Lyamuya alisema Mahakama hiyo haina mamlaka ya
kusikiliza kesi hiyo hivyo washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote
hadi watakapoitwa Mahakama Kuu.
Hata hivyo, wakili Halfan amesema
upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe
nyingine kwa ajili kutajwa.
Kesi hiyo imehairishwa hadi Januari
11, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote watatu wamerudishwa
rumande kwani kesi inayowakabili haina dhamana.
Washtakiwa hawa
watatu ni kati ya watuhumiwa saba waliotangazwa na Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya katika mkutano wa waandishi wa habari
uliofanyika tarehe 27 Disemba 2023, kuhusika na jumla ya kilo 3,182 za
dawa za heroin na methamphetamine.