Na Angela Msimbira, ARUSHA.
Serikali imefanya maboresho kwenye mfumo wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri (TPLMIS) kwa kuongeza moduli za usajili na usimamizi wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha na wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha.
Maboresho hayo yamefanywa na Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Benki Kuu (BOT) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Akizungumza jana jijini Arusha katika maonesho ya tatu ya Wiki za Huduma za Kifedha Kitaifa 2023, Ofisa Idara ya Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Kifedha kutoka Benki Kuu (BOT), Daudi Sasya amesema mfumo huu ulioboreshwa wa kielektroniki unalenga kuwezesha vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha na wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha kuwasilisha maombi ya usajili na taarifa za uendeshaji kwa njia ya kielektroniki
Amesema kuwa mfumo wa Huduma Ndogo za Fedha ni hatua ya utekelezaji wa sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017, Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na Kanuni zake Benki Kuu ya Tanzania ndio msimamizi mkuu wa vikundi inashirikiana Ofisi ya Raiis TAMISEMI , Wizara ya Fedha wameungana kwa pamoja kutoa hamasa kwa jamii kutumia mfumo wa wezesha.
Aidha, Sasya amevitaka vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha na wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha kuendelea kuwasilisha maombi ya usajili na taarifa za uendeshaji katika Halmashauri husika kupitia mfumo huo mpya ili yaweze kufanyiwa kazi na Mamlaka za Serikali za Mitaa
Naye Msajili wa Vikundi vya Kijamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Fauzia Omary amesema mfumo huo ni rafiki na wananchi wanajisajili kwenye maeneo yao na unawasaidia wanawake, vikundi na vijana kijiwekea fedha zao kwa usalama ikiwemo upatikanaji wa mikopo kupitia vikundi.


