Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Imeelezwa kuwa ugonjwa wa Homa Ya Ini miongoni mwa magonjwa yanayo ua Kimya Kimya kwani Kulingana Na Takwimu Za Shirika la Afya Dunia inaonyesha kuwa Vifo vinavyotokana na homa ya ini aina B inakadiriwa Huua Watu 820,000 Kila Mwaka na Zaidi watu millioni 296 wanaishi na maabukizi ya Virusi Vya homa ya ini aina B huku maambukizi mapya yakikadiriwa kuwa millioni 1.5 na Wengi Huishi Bila Dalili Na Kuendelea Kuambukiza Watu Wengine.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Huduma za Kitabibu Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu Dr Juma Muna wakati akizungumza katika kipindi cha Jarida kupitia Radio Bariadi Fm kilichokwenda sambamba na mada isemayo “Elimu ya Afya kuhusu ugonjwa wa Homa ya ini”
Dr Muna amesema ugonjwa wa homa ya ini ambao unasambabishwa na sababu mbalimbali lakini kwa kiwango kikubwa hasa katika maeneo yetu, bara la Afrika maambukizi Ya Virusi Wa Homa Ya Ini Ndio Sababu Kuu ya ugonjwa huu wa Homa ya ini ambapo vipo virusi aina tano ambavyo vimekuwa vikishambulia ini yaani virusi aina A,B,C,D,E huku virusi aina B na C vikichangia kwa kiwango kikubwa ugonjwa wa homa ya ini huku akibainisha kuwa virusi hivi huambukizwa kwa njia mbalimbali kupitia majimaji ya mwilini kama damu na maji maji mengine kwa njia za matumizi ya vitu vya ncha kali kama wachoraji wa tattoo, ,kujamiana ,madawa ya kulevya,kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua
Hata hivyo Dkt. Muna ameainisha kuwa pindi mhusika anapopata maambukizi haya ya virusi vya homa ya ini anaweza asionyeshe dalili awali lakini baadae huanza kuonyesha baadhi ya dalili kama Uchovu,Kichefuchefu,Mwili Kuwa Dhaifu,Homa Kali,Kupoteza Hamu Ya Kula Kupungua Uzito,Maumivu Makali Ya Tumbo Upande Wa Ini,Macho Na Ngozi Kuwa Vya Njano na Mkojo Mweusi.
Pamoja na hayo Dr Muna ametoa wito kwa jamii kuongoza mapambano dhidi ya magonjwa ya zinaa kwa kubadili mfumo wa maisha kwa kuacha tabia hatarishi ikiwepo kuacha ngono zembe,kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kuwa mwaminifu na pia matumizi sahihi ya kinga hasa kondomu ili kusaidia kujikinga na magonjwa ya zinaa ikiwepo Maambukizi ya virusi vya ukimwi,Virusi vya homa ya ini ambayo hayana TIBA pamoja na magonjwa mengine ya zinaa huku akishauri wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungulia hospitali ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Aidha Dr Muna ameishauri jamii kuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kufahamu hali zao na kuchukua hatua mapema kwani wengi wa wagonjwa wa homa ya ini hufika hospitali wakiwa katika hatua ya mwisho na hupoteza maisha ndani ya miezi michache pindi wanapofika hospitali na wengi wakiwa na changamoto kutokana na virusi vya homa ya ini ikiwepo ini kufeli na saratani ya Ini.
Mwisho Dr Muna alisisitiza umuhimu wa chanjo ya homa ya ini pindi mtu anapopima na kugundulika kuwa hana maambukizi ya virusi vya homa ya ini kuwa chanjo hiyo inamsaidia mhusika kujikinga na ugonjwa huu hatari na chanjo inafanya kazi vyema kwa mhusika kumaliza dozi zote tatu ili kufanya kazi vyema na Aliwataarifu wananchi wote wa mkoa wa Simiyu kufika viwanja vya Sabasaba Bariadi kupata vipimo vya homa ya ini,magonjwa yasiyoambukiza,magonjwa ya macho ,virusi vya ukimwi na mengine mengi BURE katika zoezi linaloendelea kuelekea kilele cha siku ya Ukimwi duniani ambapo kimkoa itafanyika viwanja vya Sabasaba Bariadi huku kauli mbiu ikisema “Jamii iongoze kutokomeza UKIMWI”