Bandung, Indonesia.
Wataalam wapatao 20
kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake wameanza rasmi mafunzo ya
kuwajengea uwezo wa masuala mbalimbali ikiwemo utafiti, usalama wa
makaa ya mawe pamoja na madini mengine katika Kituo cha Human Resource
Development Center Geology, Minerals nchini Indonesia.
Mafunzo hayo yanafanyika
ikiwa imepita takribani kipindi cha miezi sita tu baada ya kufanyika
mazungumzo na makubaliano ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali
katika Sekta ya Madini ikiwemo kuwaendeleza watumishi na wataalam
mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kumsimamia na
kuendeleza rasilimali madini.
Itakumbukwa mnano Mei,
2023 Tanzania kupitia aliyekuwa Waziri wa Madini ambaye kwa sasa ni
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Balozi wa
Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko walijadili kuhusu
kuwekeza katika shughuli za uchimbaji na ushirikiano kupitia Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya uchimbaji wa madini ya
nchini Indonesia inayoitwa Mining Industry Indonesia.
Masuala mengine
yaliyojadiliwa katika kikao hicho yalikuwa ni pamoja na fursa za mafunzo
ya shughuli za uchimbaji nchini humo ikiwemo usalama migodini.
Katika siku za awali za
mafunzo hayo, ilielezwa kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia
umekuwepo tangu mwaka 1955 ambapo Serikali ya Indonesia ilishiriki
katika ukombozi wa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na hatimaye nchi
hiyo kujenga ubalozi wake jijini Dar es Salaam mwaka 1964. Pia, Serikali
ya Tanzania ilianzisha ubalozi wake mwaka 2022 katika jiji la Jarkata
nchini humo.
Aidha, kama
ilivyobainishwa katika Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka Wa Fedha 2023/24,
miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuendeleza Madini Muhimu na Mkakati
na kuzijengea uwezo taasisi zake ziweze kutekeleza majukumu yake. Hivyo,
kufanyika kwa mafunzo hayo kunadhihirisha dhamira ya Wizara kufikia
malengo yaliyopangwa.
Aidha,
hayo yanajiri ambapo pia mafunzo mengine kwa watumishi na waatalam wa
wizara na taasisi zake wanaendelea na mafunzo yanayohusu namna ya kupata
mitaji katika miradi ya madini *(Mining Financing)* yanayofanyika
jijini Arusha.
Mafunzo hayo
yamewezeshwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na kampuni ya ASNL
Advisory Limited pamoja na ushirikiano na kampuni za Auramet
International LLC na Bankable Tanzania Limited.
Matokeo yanayotarajiwa
ni kuwawezesha maafisa wa Wizara ya Madini na taasisi zake kuwa na ujuzi
stahiki wa kuchambua, kusimamia na kukagua miradi ya uwekezaji katika
sekta na kushauri namna bora ya kiwezesha miradi hiyo kupata mitaji ya
kuwekeza ipasavyo.