SHIRIKIANENI NA WAZAZI, WALEZI NA JAMII INAYOWAZUNGUKA KULINDA USALAMA WA WANAFUNZI - NDEJEMBI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Deogratius Ndejembi amewaelekeza wakuu wa shule za msingi nchini kushirikiana na Wazazi, Walezi na Jamii inayozunguka shule zao ili kulinda usalama wa wanafunzi na kuhakikisha mnadumisha mila desturi na utamaduni wa kitanzania kwa kuwafundisha wanafunzi historia ya Tanzania na kudhibiti matendo maovu yasitokee shuleni.


Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo Novemba 8,2023 wakati wa akifungua mkutano mkuu wa Tano wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania (TAPSHA) na kuongeza kuwa pia wanapaswa kusimamia nidhamu ya Walimu na Wanafunzi Shuleni wakati wote na kuhakikisha ulinzi wa mali za shule unaimarika wakati wote.


Aidha amewaelekeza Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia na kukamilisha kwa wakati miradi yote kwenye maeneo yao kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotengwa na miongozo iliyotolewa.  

“Kwa upekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa ajira zikiwemo za walimu ambapo kwa miaka 2 pekee ameajiri jumla ya walimu 22,930 yaani walimu 9,800 kwa mwaka 2022 na walimu 13,130 kwa mwaka 2023.  Kati ya walimu hao, Walimu wa Awali na Msingi 12,801 na Walimu 10,129 ni wa Sekondari. Mwenyezi Mungu ambariki sana”amesema Ndejembi.


 Sambamba na hayo maeongeza kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu na watumishi wa kada zingine mbali mbali nchini.


“Ni matumaini yangu kuwa kazi njema inayofanywa na serikali itaendelea kuwa chachu kwenu ya kutimiza majukumu yenu kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ili kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi   wa  nchi yetu”, ameongezaa Ndejembi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde amesema kuwa somo la kingereza litaanza kufundishwa kuanzia darasa la kwanza licha ya kuwepo changamoto ya uchache wa walimu wenye umahiri wa kufundisha somo hilo.


Amesema wanafunzi hao wakianza kufundishwa somo hilo mpaka kufikia darasa la Saba watakuwa wameirika zaidi katika lugha ya kingereza jambo litakalo wasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazozipitia wanapoanza elimu ya sekondari.


“Mhe. Mgeni rasmi kama unakumbuka tulikuwa wote Njombe tulikupeleka shule moja ukajionea jinsi watoto wa darasa la tatu wanavyojua kuongea vizuri lugha ya kingereza, wanajua kujieleza na kujitambulisha vizuri,”amesema Dkt. Msonde.

Awali akisoma lisara mbele ya mgeni rasmi Mwenyekiti wa TAPSHA Rehema Ramole amemuomba mgeni kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwapa kipaumbele walimu wanaojitolea pindi ajira zinapotangazwa kwani wamekuwa wakifanya wakifanya kazi kubwa kuhakikisha watoto wanaendelea kufanya vyema katika masomo yao.


Aidha Ramole ameongeza kuwa walimu wanaendelea kupandishwa madaraja nchi nzima na elimu bure inaendelea kutolewa jambo lililoongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kuongezeka kila mwaka.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)