Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Seleman Joseph Bundala ni Kijana aliyezaliwa na Ulemavu wa Kichwa Kikubwa katika mtaa wa Kisiwani Vijibweni Kigamboni Jijini Dar Es Salaam na miongoni mwa Wanafunzi 117 wenye ulemavu katika Shule ya Sekondari Pungu pia ni miongoni kati ya wanafunzi 572, 338 wanaoanza mtihani wa Taifa wa kuhitimu Kidato cha nne leo Novemba 13, 2023.
Seleman Joseph Kijana mwenye umri wa miaka 23 ni mtoto wa Mzee Joseph Kaza Bundala mwenye asili ya Mkoa wa Tabora anayeishi Kigamboni ni kijana aliyepata majaribu mengi kwani mara baada tu ya kuzaliwa alipofikisha umri wa miezi 3 mama yake mzazi alifariki na akabaki na malezi ya baba pekee ambapo wakati mwingine alipata aibu kumlea mtoto mwenye changamoto hiyo.
“Nimezaliwa mwaka 1999 mama alifariki aliniacha nikiwa na miezi mitatu, baba akaanza kunilea, nilipozaliwa na tatizo hili baba alihangaika sana akaanza kunipeleka kwa Waganga wa Tiba Asili mara hospitalini,baadae nikakua nikaanza shule chekechea nikamaliza chekechea Hondohondo baadae shule ya msingi Salvation Army nikaishia darasa la nne nikabadilishwa kwa sababu pake hapakuwa na Special Care”amesema.
Nini maendeleo yake ya shule ya Sekondari Pugu?
Hali yangu inaendelea vizuri hapa shule ya Sekondari Pugu maana nimeanza Kidato cha kwannza mpaka kidato cha tatu nimekuwa nikifaulu vizuri sijawahi kufeli”amesema.
Mwalimu Juma Boniface ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu Manispaa ya Ilala Jijijini Dar Es Salaam amesema shule hiyo hadi sasa ina jumla ya watoto 117 wenye mahitaji maalum .
“Shule ya Sekondari Pungu ni Shule ambayo inaendeshwa kwa msingi Jumuishi wapo walemavu na wale wa kawaida, kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 117 wenye mahitaji maalum, kwa jamii ya Watanzania tulivyozoea kwa siku nyingi mtoto akionekana ana changamoto yoyote ya ulemavu anafichwa nyumbani na hawakuweza kupata nafasi ya kupata elimu , nitoe hamasa kwa jamii isiwafiche ni watoto kama watoto wengine, hawa 117 tulionao wanasoma na wanafunzi wengine wasio kuwa na ulemavu lakini kubwa zaidi wengine wanafanya vizuri zaidi na wanawazidi hata wale ambao hawana changamoto ya ulemavu” amesema Mwalimu Boniface.
Seleman anatoa wito kwa wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu.
“Wazazi wasiwafiche watoto wenye ulemavu huwezi kujua kesho atakuwa nani? Wapatiwe fursa ya elimu kama watoto wengine”amesema.
Nini suala la afya shuleni kwa wanafunzi wote ikiwemo wenye mahitaji maalum?
Mwalimu Juma anasimulia.
“Wanafunzi wote wametengenezewa mfumo wa bima ya afya ,kila mtoto wa aliyeko shule ni wajibu wa uongozi kuhakikisha kila mwanafunzi anapata bima na serikali inaleta fedha za kutosha kuhakikisha suala la lishe linazingatiwa na hawa wenye mahitaji maalum wametazamwa kwa jicho la kipekee, huduma zote kuanzia kalamu, daftari, nguo, mashuka, na lishe bora ,wale wenye watoto wenye mahitaji maalum wawalete shuleni ndio mahali salama wachangamane na jamii hadi watakapomaliza elimu yao”amesema Mwalimu Juma.
Nini ahadi yake katika Masomo hasa katika mtihani huu wa taifa wa kumaliza kidato cha nne?
Seleman anafunguka.
“Katika mtihani huu wa mwisho nitajitahidi nipate kufaulu vizuri na pia nitasoma sana”amesema Seleman.
Je, Seleman wakati anaripoti kidato cha kwanza shule ya Sekondari Pugu hali yake ilikuwaje?
Mwalimu Boniface anafafanua.
“Seleman wakati anakuja hapa shuleni hakuwa ameimarika alikuja hana uwezo hawezi kufua ,alikuwa hawezi kufanya mambo mengine kama watu wengine , kuja kwake kumemfanya aimarike achangamane na jamii lakini si kuchangamana tu na jamii, Sele sasa anafanya vizuri kwenye taaluma leo hii Sele aliyeingia hapa sio yule Sele anayeenda kuhitimu kidato cha nne na nikuhakikishie Sele atatoka na ufaulu wa daraja la kwanza au la pili ninavyomfahamu”amesema Mwalimu Boniface.
Kijana Seleman anatoa ujumbe gani kwa walimu?
Nawashukuru sana walimu mpaka naelekea kumaliza,naomba tu support katika mwendelezo wa masomo huko mbele?amesema.
Je, Seleman hushika daraja la ngapi katika mitihani yake shuleni?
Mwalimu Boniface anafafanua.
Sele anapata Division One, Two akianguka sana Division Three, kwa hiyo hilo linanipa matumaini makubwa kwa Sele kama kiongozi wake kwamba hata mtihani wa taifa anakwenda kufanya vizuri”
Na hapa baba mzazi wa Seleman Joseph Bundala aliyezaliwa akiwa na changamoto ya kichwa Joseph Kaza Bundala anasema awali alikuwa anamficha na kumfunika kichwa mtoto kwa kuogopa kuwa atachekwa kutokana na kichwa kikubwa lakini baada ya kupata ushauri kwa madaktari aliondoa unyanyapaa huo na kuwa balozi kwa wazazi wengine kuacha tabia kama hiyo kama anavyosimulia.
“Nina mtoto wa kiume alizaliwa akiwa na ulemavu wa kichwa kikubwa, na mke wangu ambaye ni mama wa mtoto alifariki mtoto akiwa mdogo sana na nilikuwa napotoshwa kuwa mtoto kama huyu hafanyi chochote nikawa namfunika kichwa kwa kuogopa kuchekwa lakini nashukuru baada ya kupata ushauri wa madaktari nikaacha tabia hiyo na maendeleo yake ni mazuri akitoka shule anafua anafagia na anaongea Kiingereza hata kama ukitoka Ulaya”amesema.
Je, Serikali hufanya nini katika utoaji wa elimu kwa jamii na kuwatambua watu wenye changamoto hii?
Johnson Mdeme ni Afisa kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma anafafanua zaidi .
“Tuna utaratibu wa kuweza kuwatambua watoto hawa pindi wanapozaliwa na changamoto ili kuweza kuzuia au kupunguza tatizo lisiwe kubwa na waweze kupata haki zao za elimu na afya bora kama watoto wengine na pia tunatoa elimu kwa wazazi katika maeneo mbalimbali na kwa kusaidiana na Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii pia kuna Programu ya Elimu ya Afya Shuleni na kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii ya Elimu ya Afya kwa Umma”amesema Mndeme.
Nini kifanyike kuzuia tatizo la kichwa kikubwa na Mgongo Wazi?
Mhe.Jabir Shekimweri ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma anafafanua.
“Tujenge tabia ya kula chakula bora , mbogamboga na matunda ,pia matumizi ya Madini ya Folic Acid ni muhimu katika kuzuia tatizo hili”amesema Shekimweri.
Seleman anatoa Msisitizo kwa Wazazi kuacha kuficha watoto wenye ulemavu.
“Nawasihi Wazazi waache tabia ya kuficha watoto wenye ulemavu maana huwezi kujua kesho atakuwa nani?amesema.
Tumtakie mtihani mwema Kijana Seleman ili aendelee na masomo mbele na mbele zaidi na tuache mila na desturi za kuwanyanyapaa watoto na badala yake kuwapeleka kupata matibabu na shule pia kama alivyosaidiwa Seleman .
MWISHO.