Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji Songea Mkoani Ruvuma.
Mhe., Dkt. Steinmeier amesema Ujerumani ipo tayari kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya vita vya Maji Maji kwakuwa kilichotokea zamani hakipaswi kusauhilka na mtu yoyote.
“Ili kuweka kumbukumbu sawa kwa sasa na kwa wakati ujao, Ujerumani tunaahidi kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho hii,” amesisitiza Mhe. Rais Steinmeier.
Mhe. Dkt. Steinmeier amesema Ujerumani inatamani kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya ‘Vita vya Maji Maji’ na kuongeza kuwa mchakato huo utahusisha vijana, wanafunzi wa shule na vyuo vikuu, wasomi na wataalamu wa hifadhi na sehemu za kumbukumbu.
Awali Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) amesema historia ya Tanzania na Ujerumani ina sura mbili tofauti. Alifafanua kuwa sura ya kwanza ni kuhusu vita waliyopigana babu zetu na sura ya pili ni yale mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Ujerumani Kama vile kujenga shule, hospitali na kutoa huduma nyingine za kijamii.
“Muhimu zaidi ni kukumbuka na kusahau yaliyopita na kuendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo na kusonga mbele kwa kuleta maendeleo kati ya mataifa yetu mawili, lakini pia katika mji wetu wa Songea ,” amesema Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa Songea wanatamani kuona makumbusho ya kisasa ya ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania yakijengwa Songea, “pia tunatamani Ujerumani itusaidie kuboresha chuo cha VETA Songea ili kuwawezesha vijana wetu kupata mafunzo mbalimbali,” amesema Dkt. Ndumbaro.
Makumbusho ya Vita vya Maji Maji ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.
Mheshimiwa Rais Stenmeier amehitimisha ziara yake ya Kikazi ya siku tatu nchini leo tarehe 01 Novemba 2023.