KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za MITAA imeipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa usimamizi mzuri wa mradi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Denis Londo wakati wa ziara ya Kamati ya kukagua miradi ya afya mkoani Lindi ukiwemo wa uboreshaji wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.
Oktoba 18, 2022, Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea ilipelekewa Sh milioni 900 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo kongwe nchini.
Uboreshaji huo ulihusisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, jengo la kufulia, jengo la kuchomea taka pamoja na njia unganishi.
Londo amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI inafanya kazi nzuri ya usimamizi mzuri wa mradi huo ambao kukamilika kwake kumekua ni faida kwa wananchi wa Wilaya hiyo ambao walikua wakikosa baadhi ya huduma.
" Tunaipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa usimamizi wake mzuri uliofanikisha kukamilika kwa mradi huu. Sisi kama wabunge tulipitisha bajeti ya fedha kwa ajili ya maboresho haya na tumeridhika na namna ambavyo thamani ya fedha imelingana na ubora wa kazi."
" Tunaipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoendelea kugusa maisha ya wananchi wake kwa kuboresha miundombinu hii ya afya," amesema Mhe Londo.