Na. WAF - Dodoma.
Katika kuendeleza juhudi za uboreshaji huduma za Afya ya Uzazi Mama na Mtoto, Serikali kupitia Wizara ya Afya inatekeleza programu ya uboreshaji huduma hizo ujulikanao kwa jina la ‘Tanzania Maternal and Child Health Investment Program (TMCHIP)’ kwa miaka Mitano ukiwa na thamani ya zaidi ya Dola Milioni 250.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokutana na Dkt. Juan Pablo Uribe, Mkurugenzi wa Afya wa Benki ya Dunia, Lishe, Idadi ya Watu na Mkurugenzi wa Ufadhili Duniani, kwenye kikao kilicholenga kujadili uboreshaji wa huduma za Afya nchini.
“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatekeleza program ya miaka Mitano kuanzia Januari 2023 hadi Disemba 2027, Programu hii inalenga kuboresha ubora wa huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto nchini”. Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema kuwa kupitia programu hiyo, Serikali itaboresha vyumba/vituo 15 vya uangalizi wa Watoto njiti (NICU) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, kuboresha NICU 10 katika vyuo vya Afya na kuboresha Vituo vya ukusanyaji wa Damu Salama Sita.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma za afya nchini kulingana na Mpango Mkakati wa tano wa Sekta ya Afya na Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano wa Tanzania.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa jitihada zinahitajika zaidi na ushiriki wa wadau katika kuboresha zaidi huduma za Afya nchini na kuomba ushirikiano wa Benki ya Dunia katika eneo la uimarishaji wa huduma kutoka kwa watoa huduma za Afya ngazi ya jamii, ugharamiaji wa Bima ya Afya kwa Wote pamoja na kuweka mifumo imara ya huduma za dharura na udhibiti wa majanga.
Kwa upande wake Dkt. Juan Pablo Uribe ameipongeza Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa kuwa na mfumo wa kusafirisha wajawazito kwa haraka kwa kutumia magari ya dharura na madereva katika jamii (M-Mama).
Mwisho, ameihakikishia Serikali kuendeleza ushirikiano katika kuboresha zaidi mifumo ya Afya, maendeleo ya watoa huduma wa afya na jitihada za kukabiliana na majanga ya Afya ya Jamii.