Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima ugonjwa wa Saratani hususan Saratani ya Matiti kwa ajili ya kujua hali zao mapema na kuanza matibabu kabla haijafika hatua ya Tatu na Nne ya ugonjwa huo.
Waziri Ummy amesema hayo leo Octoba 21, 2023 baada ya matembezi ya uelimishaji jamii juu ya Saratani yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Sweden kwa kushirikiana na Shujaa Cancer Foundation na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden.
Waziri Ummy amesema kuwa Watanzania wengi bado hawana mwitikio wa kupima Saratani ambapo amebainisha kuwa kwa mwaka ni asilimia 38 tu ya wagonjwa wa Saratani ndio wanafika katika vituo vya kutoa kutolea huduma za Afya hivyo ni muhimu wananchi kujenga desturi ya kupima Saratani mapema kabla tatizo halijawa kubwa na kuweza kupata matibabu.
“Tunao wagonjwa wengi katika majumba yetu, katika ofisi zetu, katika vijiji vyetu, mitaani kwetu ambao wana Saratani lakini hawajaweza kufika katika hospitali kwa ajili ya huduma za uchunguzi na matibabu hii imekua ni changamoto kubwa niwaombe mjitokeze kujitokeza kupima na kuweza kupata matibabu haraka”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa kila mwaka Tanzania ina wagonjwa wapya wa Saratani 42,000 ambapo wagonjwa hao wapya wanaofika kwenye vituo vya huduma za Afya ni takribani 15,900 tu.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mashine za Ultrasound hadi katika ngazi za vituo vya Afya, CT-Scan mashine kwenye kila Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na X-Ray kwa lengo la kusogeza huduma bora kwa wananchi.
Kwa taarifa,Elimu na Ushauri zaidi Piga Simu 199 Bure.
#mtuniafya #afyayanguwajibuwangu
@ummymwalimu @dr_mollel @wizara_afyatz #jaliafyayako #afyanimtaji #afyayakomtajiwako #elimuyaafyakwaumma






