Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amesema
kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau imekuja na mfumo wa kuweka vifaa vya
teknolojia ya mawasiliano kwa kupokea na kuchambua mwenendo wa majanga nchini.
Mhe. Nderiananga
ameyabainisha hayo leo Oktoba 13,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua kongamano
la maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupunguza madhara ya maafa inayoenda
sambamba na kauli mbiu isemayo “Imarisha usawa kwa uthabiti endelevu.
Aidha amesema kuwa
wameanzisha jukwaa la kijamii la kidigitali la mawasiliano ambapo wananchi
wanaweza kupokea taarifa za tahadhari za mapema kuhusu maafa au kupewa taarifa bure
kuhusu maafa katika eneo lolote.
“Kwa mfano wenye
simu zenu hapa sasa hivi, unaweza kuchukua simu yako ukaandika *190#
utaona mwenyewe itakupeleka karibu Ofisi ya Waziri mkuu inakuuliza umepatwa na
changamoto gani pengine kama ni ajali au mafuriko au mengineyo unaeleza kila
kitu hapo ili kwa pamoja tuweze kufanya kazi kwa pamoja na kwa haraka,”amesema
Mhe. Nderiananga.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mwandamizi wa World Vision Tanzania Dkt. Joseph Mayala amesema kuwa wao shirika
la kimataifa wanahakikisha viongozi wa dini wanashirikishwa katika mikakati
yote inayohusiana na suala la kukabiliana na maafa nchini kwani wana ushawishi
mkubwa katika jamii.
Naye Kaimu Mkurugenzi
wa Idara ya Manejimenti ya Maafa (RAPID) Taniel Mkongo amesema kuwa kauli mbiu
ya leo katika maadhimisho hayo inatokana na mkakati wa sendai wa kupunguza madhara
ya maafa wa 2015-2030 ambao unataka kushughulikia sababu za msingi za madhara
ya maafa.
“Tunajua kuwa mara
nyingi watu maskini na walio hatarini zaidi wanapata athari kubwa za maafa na
wanakabiliwa na athari kubwa zaidi, kupambana na kutokuwiana ni sehemu muhimu
ya kujenga mustakabali wa kustahimili kupunguza athari za maafa,”amesema.
Siku ya kimataifa
ya kupunguza maafa ilianza mwaka 1989 baada ya wito kutoka kwa Baraza la Umoja
wa Mataifa kutaka kuwepo kwa siku hii maazimio Na. 64/200 Desemba 21,2009 ilinayohitaji watu na jamii
zote duniani kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kudhibiti madhara ya maafa.